Wajasiriamali wapewa mbinu za kufanikiwa

Meneja Mkuu wa Kampuni ya KPMG, James Chotamawe akizungumza wakati wa kongamano la wajasiliamali na wafanyabiashara wa kati jijini Dar es salaam.

Dar es Salaam. Meneja wa usimamizi na uangalizi wa mifumo inayotoa taarifa wa kampuni ya uhasibu ya KPMG James Chotamawe, amewataka wajasiriamali wachanga, wadogo na wa kati (MSMEs) kuweka utaratibu wa kuwa na taarifa sahihi za biashara zao.

Chotamawe ametoa wito huo leo, Alhamisi, Aprili 27, 2023 jijini Dar es Saalm katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki kunakofanyika kongamano la wajasirimali lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Commmunications Limited (MCL) linalojadili namna ya kuwezesha biashara changa, za chini, ndogo na za kati kukua haraka.

Chotamawe ambaye alizungumzia umuhimu wa matumizi ya uchambuzi wa kitakwimu katika kutabiri hali ya biashara kwa siku zijazo na kuongeza faida.

Amesema katika ulimwengu wa sasa data ndicho kitu chenye thamani kuliko vingine vyote kwani kampuni kubwa za Google na Microsoft, biashara yao kubwa sasa ni uuzaji wa taarifa kwa ajili ya kusaidia matangazo katika biashara.

“Asilimia kubwa ya faida ya mitandao ya kijamii inatokana na matangazo ambayo ni kwa kuuza taarifa. katika kampuni, biashara zetu kitu muhimu ni kuhifadhi taarifa za tabia ya wanunuzi kwani hizo ndizo zitakuonyesha namna gani unaweza kukuza biashara yako na kutabiri mwenendo wa biashara kwa siku zijazo,” amesema

Amezungumzia ni muhimu kuwa na taarifa sahihi katika kukuza ujasirimali kwa sababu zinasaidia kujua ni bidhaa gani inayopaswa kutiliwa mkazo katika biashara yake kwa lengo la kuongeza biashara na faida.

Ametolea mfano wa suala la ndoa akisema ukiona zimeongezeka mwezi huu ni kwamba ndani ya mwaka mmoja nguo za wajawazito zitaongezeka ndani ya mwaka mmoja na ndani ya miaka mitatu ijayo kutakuwa na uhitaji wa shule za chekechea.

“Kwa kupata taarifa za mwenendo uliopo na kutabiri kesho ni rahisi kupanga namna gani unaweza kunufaika na fursa zilizopo kwa siku zijazo lakini pia inasaidia kukupa njia za kufanya ili kuepuka kuweka mtaji wake hatarini,” anasema

Chotamawe amesisitiza kuwa ni muhimu kuwa na taarifa na kuzichakata, kutabiri manunuzi ya wateja kwa siku zijazo na kusaidia kufanya maamuzi ndiyo maana baadhi ya maeneo ya biashara na huduma wanaomba maoni ya mteja baada ya kumhudumia.

Kongamano la MSMEs linaendelea hivi sasa katika ukumbi wa wa The Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, limedhaminiwa na Benki ya CRDB, Kampuni ya usafirishaji ya DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media, Kampuni ya matangazo ya Ashton na ukumbi wa mikutano wa The Dome.