Wakesha kusubiri uzinduzi kituo cha afya

Muktasari:

  • Wananchi katika Kijiji cha Tyegelo, Wilaya ya Iramba wamekesha wakisubiri kuzinduliwa Kituo cha Afya Tyegelo.

Iramba. Wananchi katika Kijiji cha Tyegelo, Wilaya ya Iramba wamekesha wakisubiri kuzinduliwa Kituo cha Afya Tyegelo.

Wananchi hao wamesema ni vema wakajengewa na barabara kwani pamoja na kukamilika kwa kituo hicho, huenda vifo vikaendelea kutokea kutokana na kukosa uhakika wa mawasiliano ya barabara, hasa nyakati za mvua za masika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao akiwemo Christina Richard, amesema mvua zikinyesha, mito inafurika maji na kushindwa kupita.

Shibeda Magoma amesema kabla ya kituo hicho walikuwa wanateseka kuwabeba wagonjwa kuwapeleka hospitali ya Wilaya ambayo ni zaidi ya kilometa 40 kutoka wanapoishi.

Kwa upande wake Mratibu wa afya ya Uzazi na Mtoto Wilayani Iramba, Celina Jumanne, alikiri kupokea vifo vilivyotokana na wagonjwa kucheleweshwa kufikishwa hospitalini au kufika wakiwa katika hali mbaya.

Akizindua kituo hicho, Mkuu wa Wilaaya ya Iramba, Suleiman Mwenda aliahidi kutengenezwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kueleza tayari wamepokea Sh3.5 bilioni na kuona waanze kwanza kujengae makaravati.