Wakristo watakiwa kuishi katika amani ya kudumu

Muktasari:
Wakristo nchini wametakiwa kutafakari na kisha kukabidhi maisha yao kwa Yesu Kristo aliyebeba amani ya kudumu ikiwa na majibu ya changamoto wanazopitia
Dar es Salaam. Msaidizi wa Askofu Kanisa Kuu la Kanisa KKKT Azania Front jijini Dar es Salaam, Chediel Rwiza amewataka wakristo nchini kukabidhi maisha yao kwa Yesu Kristo aliyebeba amani ya kudumu ikiwa na majibu ya changamoto zao.
“Huwezi kutafuta amani bila kumtafuta Yesu Kristo iwe kwa familia, Taifa au duniani kote,” amesema Askofu Rwiza jana Alhamisi Desemba 24, 2020 katika ibada ya usiku mtakatifu wa kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristo.
Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Dk Alex Malasusa, kiongozi huyo wa dini alitumia kitabu cha Mathayo kueleza mazingira magumu aliyokuwa nayo Bikira Maria mbele ya familia, mchumba wake Yusuph na jamii yake.
“Aliwaza adhabu ya kupigwa mawe hadi kufa, aliwaza aibu kwa familia yake lakini roho mtakatifu alipatia amani, sisi tunapopita kwenye magumu nani anatusaidia? Faraja yetu inakuwa nani, "alihoji Askofu Chediel.
Katika ufafanuzi wake alimtaja Yesu kuwa na amani ya kudumu, mwokozi kutoka katika dhambi na hakuna jambo atafanikiwa binadamu bila kumtegemea yeye.
“Leo sio kwamba tunashuhudia tu kuzaliwa ila tunaona unabii ukitimia, tukabidhi maisha yetu, familia na koo zetu wakati huu Yesu anapozaliwa,” alisema.