Wakulima wauza korosho shingo upande

Meneja Mkuu wa chama kikuu cha ushirika cha Tandahimba &Newala cooperative union (TANECU) Mohamed Mwinguku akizungumza jambo wakati wa mnada wa kwanza wa korosho wa chama hicho uliofanyikia Wilayani Tandahimba leo. Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Katika mnada huo, zaidi ya kampuni 36 zimejitokeza kununua korosho japo inadaiwa kuwa wakulima wameuza korosho hizo kwa shingo upande.
Mtwara. Zaidi ya tani 16,000 za korosho zimeuzwa katika mnada wa kwanza huku bei ya juu ikiwa ni Sh2, 050 na bei ya chini ikiwa ni Sh1,900.
Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu) chenyewe kimeuza kwa bei ya kati ya Sh2, 050 na Sh1, 950; huku kile cha Mtwara na Masasi (Mamcu) kikiuza kati ya Sh2, 031 na Sh1, 900.
Katika mnada huo, zaidi ya kampuni 36 zimejitokeza kununua korosho japo inadaiwa kuwa wakulima wameuza korosho hizo kwa shingo upande.
Akizungumza mara baada ya mnada huo kuisha, Bibie Fadhili ambaye ni mkulima wa korosho kutoka Wilaya ya Tandahimba, mkoani hapa; amesema kuwa wameuza korosho hizo shingo upande kwani hawajaridhika na bei hizo.
“Mimi kama mkulima sijaridhika na bei ila hatuna jinsi tulitarajia angalau mkulima apate Sh2000, tunasomesha watoto sasa tukipata Sh1, 500; kusomesha watoto vyuo vikuu. Kwa sasa hali ni ngumu kwetu, yaani hiyo Sh2, 050 makato mkulima atapata Sh1, 500 Serikali ikae itufikirie sisi wakulima,” amesema Bibie na kuongeza;
“Kwa kweli hii bei imepita na wakulima tumeuza lakini hatuna namna wala hatuna ujanja yaani viwatilifu vililetwa na tulipewa bure lakini tunagharama za kupalilia, kupulizia na kuokota zote zinaishia kwenye hiyo pesa, mkulima hakuna anachopata hapo.”
Kwa upande wake Ahmed Alfan, mkulima kutoka katika kijiji cha Nanyanga, wilayani Tandahimba; amesema kuwa japo wamekubali kuuza korosho zao, lakini bei hiyo haina maslahi kwao na kwamba serikali ione namna ya kupunguza ushuru ili wapate faida katika kilimo hicho.
“Kwa maslahi bei hii ni ndogo na haifai tunaomba serikali itusaidie kwenye hili ikiwezekana wapunguze tozo angalau ingekuwa Sh2, 500 ili mkulima apate Sh2, 000 tumeuza lakini hatuna namna,” amesema Alfan.
Mwenyekiti wa Mamcu, Siraji Mtenguka amesema: “Kwakweli tumeuza tu lakini bei hazifurahishi, tatizo ni kwamba tunauza korosho ghafi sio zilizobanguliwa, huwezi leta maringo yaani hatuwezi kulimudu soko kwa kuuza korosho ghafi.”
Nae Meneja Mkuu wa Tanecu, Mohamed Mwinguku amesema kuwa chama hicho kimepeleka tani 7752 sokoni na kwamba zimeuzwa zote ambapo zaidi ya kampuni 36 zimejitokeza katika mnada huo.
"Tumeuza korosho bei juu ni Sh2, 050 na bei ya chini ni Sh1, 950 ambao mwitiko wa wanunuzi umekuwa mkubwa. Tulikuwa na wanunuzi 36 kati ya 46 walioandika barua za kuomba kununua 46, hi ini tofatui na msimu uliopita ambapo wanunuzi walikuwa chini ya 25,” amesema.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tanecu, Karim Chipola amesema kuwa baada ya kuchakata bei wamekubaliana kuuza korosho kwa bei hizo...wauzaji ni wakulima nilifikisha kwao nao kwa umoja wao wamekubalina kuuza korosho hizo ambapo kikubwa wanapaswa kusimamia ubora wa korosho.