Walimu 13,000 waajiriwa, wenye umri mkubwa wapewa kipaumbele

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imekamilisha ajira za walimu 13,000 na tayari wameshapangiwa vituo vya kazi wanakotakiwa kuripoti kuanzia Desemba mosi, 2020.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imekamilisha ajira za walimu 13,000 na tayari wameshapangiwa vituo vya kazi wanakotakiwa kuripoti kuanzia Desemba mosi, 2020.

Akizungumza jijini Dodoma leo Ijumaa Novemba 27, 2020 katibu mkuu ofisi ya rais Tamisemi, Joseph Nyamhanga amesema ajira za walimu hao ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais John Magufuli Septemba 7, 2020.

Nyamhanga amesema walimu walioajiriwa ni waliojitokeza na kuomba wenyewe moja kwa moja na kipaumbele kikubwa walipewa wenye umri mkubwa.

“Pamoja na yote lakini tumezingatia umri kwa waombaji kwani mnajua mwisho wa umri wa mwisho kuajiriwa ni miaka 45 hivyo mfumo ulitazama pamoja na mambo mengine wenye umri unaokaribia na huo,” amesema Nyamhanga.

Walimu walioajiriwa ni wenye elimu ya astashahada, stashahada na wenye shahada katika masomo kiingereza, uraia, jiografia na kiswahili na wengi wao wamepangwa kufundisha shule za msingi.

Amesema muda wa walimu hao kuripoti ni Desemba 1 hadi 15, 2020 na baada ya hapo itakuwa ni mwisho wa kuwapokea,  watakaoshindwa katika muda huo watakuwa wamejiondoa wenyewe katika mfumo.