Waliohama Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera wafikia 3,822

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi akizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni mkoani Tanga leo. Picha na Sunday Geoerge

Muktasari:

Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi amesema wananchi 100,015 ndio walikuwepo ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na kati yao 3,822 tayari wamehamishwa kwa hiari.

Handeni. Serikali ya Tanzania imesema hadi sasa wakazi 3,822 waliokuwa na makazi ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa Ngorongoro na mifugo yao 18,102 wamehamia tarafa ya Msomera wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

Hadi kufikia Machi 2024, Serikali imeweka lengo la kuwahamisha watu 20,000 kutoka ndani ya hifadhi hiyo, kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.

Matinyi amesema hayo leo Jumatano Janauri 17, 2024  wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Msomera, wilayani Handeni yalipo makazi yalijengwa na Serikali kwa ajili ya wananchi hao.

Waandishi wa habari wamefika Msomera kujionea maisha ya wananchi na kazi inayofanywa na Serikali ya kujenga makazi na pia katika Hifadhi ya Ngorongoro kuona maisha ya wengine waliosalia wakichangamana na wanyama kupitia shughuli zao.

"Uhamishaji wa wananchi umefuata utaratibu, kila mtu anajua mambo yanayoendelea kuhusu kuwahamishia maeneo yaliyotengwa. Kuna upotoshaji unaendelea kuwa kuna ukiukaji wa haki za binadamu kwenye zoezi hili, wakisema kuna watu wanapigwa ili wahame, niwahakikishie hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu unafanyika katika utekelezaji wa shughuli hii," amesema Matinyi.

Matinyi amesema uondoaji wa wananchi hao hifadhini ni kwa lengo la kuwaboreshea maisha na kuendeleza uhifadhi wa Ngorongoro ambao unaingia kwenye hatari ya kutokomezwa na idadi ya mifugo inayoongezeka ndani ya hifadhi.

Ameeleza kuwa watu wanaopinga hatua hiyo ya Serikali kuwahamisha wananchi hawajui ukweli wa maisha ya wananchi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

"Licha ya upotoshaji unaofanyika na wanaharakati, hakuna aliyekwenda kufungua kesi mahakamani kupinga kinachoendelea kwa sababu hawana sababu, ili mtu aipeleke Serikali mahakamani lazima awe na ushahidi, hawana ushahidi. Niwahakikishie hakuna hata sehemu moja Serikali itatumia nguvu kwenye zoezi hili au kukiuka haki za binadamu," amesema.


Ongezeko la watu

Mwaka 1959 Serikali ilianzisha Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ikiipa hadhi ya kukaliwa wanyama na binadamu.

Hatua hiyo iliifanya Serikali kuwahamisha wananchi 4,000 waliokuwa wakiishi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwenda Ngorongoro.

Kwa takwimu za Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro baada ya wananchi hao kujumuishwa pamoja na waliokuwepo idadi yao ilikuwa 8,000 na mifugo 200,060, lakini mwaka 2017 idadi ya wananchi ilikuwa imeongezeka kufikia hadi 100,010, jambo ambalo liliendelea kuhatarisha eneo la hifadhi.

Matinyi amesema endapo Serikali isingechukua hatua ya kuondoa wananchi hao kwa utafiti uliofanyika, kufikia 2050 Hifadhi ya Ngorongoro ingetoweka.

Amesema eneo la hifadhi ni kilomita za mraba 8, 292 na eneo wanalokalia wananchi ni kilomita za mraba 3,700 embalo linaendelea kuongezeka kutokana na idadi ya watu kuongezeka.

Kufuatia uondoaji wa wananchi hao Serikali inakusudia kufanya mabadiliko ya Sheria ili Mamlaka hiyo ibaki na kusimamia uhifadhi pekee bila kuwepo kwa shughuli za watu ndani ya hifadhi.

Maisha Msomera

Diwani wa iliyokuwa kata ya Kakesyo ndani ya Ngorongoro, Johanes Tiamasi ambaye sasa yupo Msomera, amesema wananchi hawajagoma kuhama ndani ya hifadhi bali ni mazoea.

"Hakuna hofu ya kuhama, bali watu wamezoea makazi yao, nyumbani ni nyumbani hata kama ni juu ya mti, hivyo waendelee kuhamasisha, wengine tunawasiliana nao tunawaeleza hali ilivyo huku, ni ukweli wananchi kule wapo kwenye makazi duni, huku watu wana wigo mpana wa kufanya shughuli za maendeleo, tofauti na wanakaoishi sasa," amesema.

Mzee Saiboku Laiza aliyepo pia Msomera, amesema mazingira waliyokuwa wakiishi Ngorongoro hayakuwa na uhuru kama ilivyo sasa.

"Huku tunalima na chakula kipo, tofauti na Ngorongoro ambako shughuli kubwa ni ufugaji tu na hakuna kufanya shughuli yeyote ya maendeleo, ni muhimu wenzetu wakapewa elimu ya kutosha kwa sababu hiyo ndio inawakwamisha kufanya maamuzi ya kuja Msomera," amesema

Uhuru anaouzungumzia Mzee Saiboku, anasema walipokuwa wakiishi ndani ya hifadhi hawakuruhusiwa kufanya uendelezaji wa nyumba zao na muda wa kutotoka nje ya hifadhi ni saa 12 jioni, jambo ambalo liliwarudisha nyuma kiuchumi.

Mkazi mwingine, Sara Yohana amesema eneo la Msomera kwake ni fursa kutokana na uwepo wa eneo kubwa linalofaa kwa kilimo.

"Mashamba tuliyopata ni sehemu ya kuendeleza maisha ya jamii ya Wamasai, elimu kwa wenzetu iendelee kutolewa kuwashawishi wenzetu waje huku tuishi," amesema

Akizungumzia hatua iliyofikiwa kuwahamisha wananchi hao, Ofisa Uhusiano Mwandamizi Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Kassim Nyaki amesema hadi kufikia Januari 15, 2024 kaya 1,069 zimejiandikisha kuhama kwa hiari.

Kwa awamu ya pili kufikia Januari 12, 2024 tayari  kaya 525 zilijiandikisha kuhama na kaya 126 zenye watu 812 na mifugo 2,581 zilihamishwa kwenda Msomera na maeneo mengine.


Maisha mapya

Wanaohama kutoka Hifadhi ya Ngorongoro hujengewa nyumba,  wanapewa ardhi ekari mbili na nusu za kilimo na ekari tano eneo la malisho pamoja na Sh10 milioni hadi Sh15 milioni.

Shughuli za kuhama zilianza Februari mwaka 2022, Serikali ilipoanza kuelimisha na kuhamasisha watu walioridhia kujiandikisha na kuhama Ngorongoro.