Wanachama Chadema wasema mchuano wa Sugu na Msigwa umeonesha ukomavu
Muktasari:
- Wanachama wa Chadema wamesema kwa sasa chama hicho kimekua na kinaweza kujiendesha bila kumtegemea mtu mmoja.
Njombe. Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamesema upinzani uliooneshwa na Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na Mchungaji Peter Msigwa katika uchaguzi wa ngazi ya uenyekiti Kanda ya Nyasa, unaakisi kukua kwa chama hicho ndani na nje.
Uchaguzi huo uliofanyika jana Mei 29 2024 Makambako, mbali na upinzani katika nafasi mbalimbali, lakini kiti cha mwenyekiti kilikuwa moto baina ya wagombea hao wawili.
Sugu ambaye alikuwa anagombea nafasi hiyo kwa mara ya kwanza, alishinda kiti hicho kwa kura 54 akimtupa aliyekuwa anatetea nafasi hiyo, Mchungaji Msigwa aliyepata kura 52.
Wafuasi wa Chadema na wananchi wengine wakiwamo wa vyama vingine macho na masikio yao yalikuwa ni kujua nani ataibuka mshindi kutokana na nguvu ya ushawishi kwa makada hao ndani na nje ya chama.
Msigwa ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini licha ya kubwagwa katika uchaguzi huo, alionesha kukubaliana na matokeo, huku akiahidi kushirikiana na uongozi mpya.
“Sikuja Chadema ili niwe kiongozi, nawashukuru na kuwapongeza kwa uamuzi, nitaendelea kuwa pamoja na viongozi wapya na nimpongeze Sugu kwa ushindi,” amesema Msigwa.
Mwanachama wa chama hicho, Ahad Mtweve amesema ushindani wa vigogo hao ulianza mapema kabla ya uchaguzi na kusababisha wapigakura kukosa pa kuegemea.
“Hii inatuonesha hata uchaguzi ujao Serikali za mitaa na ule Mkuu wa 2025, Chadema tunaweza kuongoza sehemu zote hata kuchukua dola, Sugu na Msigwa ni watu wenye nguvu” amesema Mtweve.
Naye Ruty Tamalu kada wa chama hicho, amesema walitarajia matokeo ya aina yoyote kutokana na nguvu za waliokuwa wagombea na kwamba Chadema ya sasa ni kubwa.
“Uchaguzi ulikuwa wa haki na tuliamini mmoja atashinda, ila kwa mtifuano ulivyokuwa imeonesha wazi Chadema ya sasa siyo ya miaka mitano nyuma, tunaweza kuishi bila mtu fulani,” amesema Ruty.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Sugu amesema kwa sasa jukumu kubwa itakuwa ni kuunganisha wanachama na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi ujao kupambana na Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Chama ndicho kimeshinda, kunipitisha mimi inamaanisha mlikubaliana na hoja zangu 10, hivyo mwenyewe tu siwezi bali kwa ushirikiano, ili niwe bora lazima nipate mwenyekiti wa mkoa, wilaya na majimbo walio bora” amesema Sugu.