Wanafunzi 30 wanusurika kifo baada ya bweni kuteketea Uyui

Bweni la Wavulana Shule ya Sekondari Ilolangulu iliyopo Wilaya ya Uyui likiwa limeungua pamoja na vitu vilivyokua ndani, katika tukio la moto huo wanafunzi wakiwa wanajisomea darasani. Picha na Johnson James
Muktasari:
- Moto huo umeteketeza bweni moja wanalolala wanafunzi wa kiume likiwa na vitu vyao vyote.
Uyui. Zaidi ya wanafunzi 30 wa kidato cha pili na cha nne katika Shule ya Sekondari Lolangulu, iliyopo Uyui mkoani Tabora, wamenusurika kifo baada ya bweni lao kuwaka moto usiku wa Julai 25, 2024, na kuunguza samani na mali zao.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 26, 2024, mkuu wa shule hiyo, Justine Machage, amesema moto huo ulizuka saa 3 usiku wa Julai 25, 2024 wakati wanafunzi hao wakiwa wanajisomea darasani.
“Hapa shuleni tuna programu ya makambi kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne ambao wanafanya maandalizi ya mitihani ya Taifa. Wakati wakiwa darasani, moto ukazuka na kuunguza bweni lote.
“Baada ya moto kuwa mkubwa, kelele zikapigwa. Kwa kuwa nilikuwa hapa shule, nilifika na kunyofoa waya wa umeme kwenye swichi, ndipo nikaruhusu wanafunzi kuuzima kwa kutumia mchanga na maji kwa kuwa umeme tuliukata kwa shule nzima,” amesema Machage.
Ashura Simba, mwanafunzi wa kidato cha nne katika sekondari ya Lolangulu, amesema taarifa za moto huo walizipata kupitia mwanafunzi aliyekuwa ametoka msalani, ndipo kelele za msaada zilipoanza kusikika.
“Sisi tulikuwa tunajisomea. Wakati tukiendelea na masomo, mwanafunzi mwenzetu aliyekuwa ametoka msalani akaanza kupiga kelele kwamba bweni la wavulana linawaka moto. Tukatoka na kuanza kushirikiana kuuzima,” amesema Simba.
“Madaftari ya wanafunzi wenzetu yaliungua yote, nguo zao ziliungua na hawana chochote kwa sasa. Tunawaomba wadau na serikali watusaidie kupata mahitaji kwa wenzetu maana hawana pa kulala na mahitaji mengine, moto uliunguza kila kitu,” ameongeza Simba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Said Ntahondi, amesema moto huo umesababisha hasara kwa wanafunzi na taharuki kubwa kwa wazazi.
“Baada ya kutokea ajali ya moto, kulitokea taharuki kwa wazazi kudhani watoto wao wameungua kwenye shule hii, lakini tulihakikisha moto umezimwa na wanafunzi wote wako salama,” amesema Ntahondi.
Kwa upande wake, Neema Mfugale, Katibu Tawala Wilaya ya Uyui, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Zacharia Mwansasu, amesema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.
“Chanzo cha moto ni hitilafu ya umeme na tayari tumeanza kuchukua hatua kwa mafundi kupitia upya mfumo wa umeme ili changamoto hizi zisijirudie.
“Tunawaomba wazazi wawe watulivu, watoto wao wako salama. Baada ya moto kuzuka, wanafunzi zaidi ya 30 walipoteza vitu vyao muhimu kama sare za shule, viatu, madaftari, nguo, pamoja na magodoro.
“Sisi kama serikali tumepeleka magodoro 30, madaftari zaidi ya 260, ndoo za kuogea, na mahitaji mengine ili wanafunzi waendelee na masomo yao kama kawaida,” amesema Mfugale.