Wanafunzi 400,000 kunufaika na Sh115 bilioni Zanzibar
Muktasari:
Wanafunzi 400,000 wa shule za msingi visiwani Zanzibar, nusu yao wakiwa wasichana wanatarajiwa kunufaika na miundombinu bora ya elimu ambayo itawasaidia kujiunga na masomo ya sekondari, baada ya Benki ya Dunia kuidhinisha mkopo chini ya Mradi mpya wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Msingi Zanzibar (ZIQUE).
Dar es Salaam. Zaidi ya wanafunzi 400,000 wa shule za msingi visiwani Zanzibar nusu yao wakiwa wasichana wanatarajiwa kunufaika na miundombinu bora ya elimu ambayo itawasaidia kujiunga na masomo ya sekondari, baada ya Benki ya Dunia kuidhinisha mkopo chini ya mradi mpya wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Msingi Zanzibar (ZIQUE).
Mkopo huo wa Dola milioni 50 sawa na Sh115 bilioni kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA) umepangwa kuboresha stadi za ujifunzaji na kuondoa pengo la jinsia katika elimumsingi visiwani humo.
Desemba 22, 2022 kupitia taarifa iliyosamba kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Nathan Belete amesema, "Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kutoa fursa ya elimu ya msingi kwa wote," amesema.
Hata hivyo, amesema ili kuongeza ukuaji wa sekta ya elimu na na kuondoa umaskini ifikapo mwaka 2050 visiwani Zanzibar, uwekezaji mkubwa unahitajika ili kuboresha matokeo ya msingi ya ujifunzaji.
Serikali ya Zanzibar ilifuta ada kwa shule za awali na msingi mwaka 2015 na sekondari mwaka 2018 hatua iliyochangia ongezeko la udahili katika skuli za serikali zinazochukua zaidi ya wanafunzi 467,000.
Ili kuhakikisha wanafunzi wote wanasonga mbele kupitia mfumo wa elimu wenye viwango vya kutosha vya kujifunza, ZIQUE itasaidia kutatua changamoto za sekta ya elimu kupitia mchakato na mabadiliko ya sera katika mfumo wa elimu ambayo yatasaidia kuimarisha ubora wa utoaji wa huduma.
Mtaalamu wa Uchumi na Elimu mwanadimizi wa Benki ya Dunia Tanya Savrimootoo amesema,"Huu ni ubunifu mzuri wa ZIQUE, kupeleka mfumo wa skuli kwa ajili ya utoaji wa maendeleo endelevu ya kitaaluma (CPD);
Matumizi ya teknolojia kwenye elimu ili kuimarisha ufundishaji kwa wanafunzi na mwalimu CPD na tathmini kubwa ya ujifunzaji, itaruhusu Serikali kufuatilia kwa kutoa ripoti kuhusu matokeo ya ujifunzaji na kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto za ujifunzaji,” amesema.
Mradi wa ZIQUE unawalenga wanafunzi wanaoishi na ulemavu wa macho, kupitia utengenezaji wa vifaa vya kujifunzia.
Wengine watanufaika kupitia muundo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na shule mpya.
Pia ZIQUE itawanufaisha zaidi ya walimu 13,000 wa Shule za msingi na sekondari za serikali (69% kati yao wakiwa wanawake) na zaidi ya walimu wakuu 520 katika mfumo wa shule za umma