Wanafunzi 7,297 kati ya 8,292 hawajaripoti kidato cha kwanza Mjini Geita

Mkuu wa Wilaya ya Geita Cornel Magembe akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madarasa saba na ofisi mbili za walimu yaliyokarabatiwa na Kampuni ya Blue Coast Investment katika Shule ya Msingi Nyamalembo iliyopo mjini Geita.
Muktasari:
- Wanafunzi 5,217 waliopaswa kuripoti kidato cha kwanza kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni 1,200 pekee ndio walioripoti
Geita. Wanafunzi 995 sawa na asilimia 12 kati ya wanafunzi 8,292 waliopangwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari katika Halmashauri ya Mjini wa Geita wilayani Geita ndio walioripoti shule hadi sasa.
Wakati wanafunzi 7,297 wakiwa hawajaripoti kwa shule za halmashauri ya Mji wa Geita, wanafunzi 5,217 waliopaswa kuripoti kidato cha kwanza kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni wanafunzi 1,200 pekee sawa na asilimia 23 ndio walioripoti.
Kwa darasa la kwanza Halmashauri ya Mji walikadiria kuwa na watoto 10,000 na walioripoti ni 9,123 huku Halmashauri ya Geita ilitarajia kuwa na wanafunzi 34,000 na hadi sasa walioripoti ni 24,577sawa na asilimia 71 .
Kwa upande wa darasa la awali Halmashauri ya Mji ilikadiria kuandikisha watoto 11,631 na hadi sasa walioripoti ni 8,320 sawa na asilimia 72 huku Halmashauri ya Wilaya wakiripoti wanafunzi 20,680 sawa na asilimia 54 ya watoto 38,219 waliotarajiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amewataka wazazi wenye watoto wanaotarajia kuanza shule kutoendelea kukaa nao nyumbani kwa kisingizio cha kukosa mahitaji.
Akizungumza wakati wa kupokea madarasa saba na ofisi mbili za walimu katika Shule ya Msingi Nyamalembo zilizokarabatiwa na Kampuni ya Blue Coast Investment, mkuu huyo wa wilaya amewataka wanafunzi hao kuripoti shule na waendelee na masomo wakati wazazi wakiendelea kuwatafutia mahitaji muhimu kama sare na vifaa vya kujifunzia.
Pia, amepiga marufuku walimu kutowarudisha watoto watakaohudhuria shule wakiwa na nguo ambazo sio rasmi kwa shule na kuwataka wawapokee na kuwapa ushirikiano kama wanafunzi wengine hadi pale wazazi wao watakapo wakamilishia mahitaji muhimu.
Meneja wa Blue Coast Investment Jeremia Musa amesema kampuni hiyo itaendelea kuangalia miradi yenye uhalisia wa kimaendeleo hasa katika sekta za elimu na afya.
Amesema katika kukarabati madarasa hayo saba na ofisi mbili wameweka sakafu,madirisha na kupaka rangi ndani na nje kwa Sh43.6 milioni.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamalembo, Josia Emanuel amesema kukarabatiwa kwa madarasa hayo kutasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kupunguza utoro kwa wanafunzi.
Monica Charles mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo amesema awali walisoma kwenye vumbi na kuchafuka lakini ukarabati uliofanyika utawasaidia wasome kwenye mazingira bora na rafiki.