Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi mazingira magumu wasaidiwa taulo za kike

Katibu wa Mbunge wa Vunjo, Gulatone Masiga,  akimkabidhi taulo za kike mwalimu wa shule ya Sekondari Mboni, Mwalimu Magdalena Kiwale kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo hilo, Dk.Charles Kimei. Picha na Janeth Joseph.

Muktasari:

 Msaada huo wa taulo umetolewa na  Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei ili kuimarisha mahudhurio.

Moshi. Wanafunzi wa kike zaidi  ya 1, 440 wanaotoka katika mazingira magumu katika jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro,  wamepatiwa taulo za kike bure na Mbunge wa jimbo hilo, Dk Charles Kimei ili kuimarisha mahudhurio shuleni.

Baadhi ya wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu hasa ya vijijini, wamekuwa wakishindwa kuhudhuria baadhi ya vipindi darasani wawapo kwenye siku zao za hedhi kwa kukosa taulo za kike ili kujisitiri.

Akikabidhi taulo za kike kwa baadhi ya shule za jimbo hilo kwa niaba ya mbunge wa jimbo hilo, jana Machi 10, 2024,  Katibu wa mbunge, Gulatone Masiga amesema watakabidhi taulo za kike kwa shule zote 30 za jimbo hilo.

"Leo (jana) tunafanya makabidhiano ya taulo za kike kwa baadhi ya shule zetu, lengo kuhakikisha mabinti zetu hawapati changamoto ya kukosa masomo na fedheha wanapokuwa kwenye siku zao za hedhi.

"Mbunge ameona ni vyema kutoa taulo hizi kwa shule zote 30 kwa sababu wapo baadhi ya wanafunzi walishawahi kuja ofisini hapa, kuomba msaada wa pedi, hivyo kila shule wanafunzi 48 watapatiwa msaada huu wa pedi," amesema Masiga.

Nao baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya sekondari, Mieresini iliyopo jimbo la Vunjo, wamesema baadhi yao wanashindwa kuhudhuria vipindi darasani kwa kukosa taulo za kike,  na hivyo kulazimika kubaki nyumbani mpaka hapo watakapomaliza siku zao za hedhi.

Nasra Chilwa, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, alisema changamoto ya utoro darasani inasababishwa na baadhi yao kushindwa kupata huduma ya taulo za kike, hivyo hulazimika kubaki nyumbani kwa kukosa msaada. 

"Tunamshukuru mbunge kwa msaada huu aliotupatia wa taulo za kike, kabla ya hapo tulikuwa tukipata changamoto mbalimbali. Wengine wanashindwa kuhudhuria vipindi darasani kwa kukosa pedi.

"Tunaamini mahudhurio yatakuwa mazuri shuleni na tutafaulu kwa kiwango kinachotakiwa. Hakutakuwa na kisingizio chochote cha mwanafunzi kushindwa kuhudhuria vipindi," amesema.

Naye Norah Kanje, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mieresini, amesema kutokana na baadhi yao kukosa fedha za kununulia pedi wanalazimika kutumia vitambaa kujisitiri, hali ambayo inawafanya kushindwa kujiamini wawapo kwenye siku zao, hivyo kukata tamaa ya kuhudhuria vipindi.

Mwalimu wa shule ya Sekondari Mboni, Magdalena Kiwale, alimshukuru Dk Kimei kwa kujitolea kuwasaidia watoto wa kike,  kwa kuwa wanapitia katika changamoto nyingi wakati wakiwa kwenye siku zao za hedhi.

"Tunamshukuru Mbunge kwa kuona tatizo hili la wanafunzi wetu wa kike, kiukweli watoto wetu hawa wamekuwa wakipata changamoto mbalimbali hasa wale wanaotoka katika mazingira magumu, maana uwezekano wa kupata hizi taulo ni mgumu sana," amesema.