Wanajeshi wachangamkia chanjo ya Uviko -19

Muktasari:
- Mkuu wa Hospitali Kuu ya Kijeshi Lugalo, Brigedia Jenerali Fredi Kivamba amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wafanyakazi kada ya jeshi kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19.
Dar es Salaam. Mkuu wa Hospitali Kuu ya Kijeshi Lugalo, Brigedia Jenerali Fredi Kivamba amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wafanyakazi kada ya jeshi kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19.
Brigedia Jenerali Kivamba amebainisha hayo leo Ijumaa jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya Chuo cha Kijeshi cha Sayansi za Tiba Lugalo.
Amesema moja ya sababu ya kada hiyo kuchangamkia chanjo ni kutokana na jeshi hilo kufanya kazi na mataifa mbalimbali ya nje ya nchi ambayo moja ya masharti yaliyoweka ili watu waweze kuingia katika nchi zao lazima wawe wamepata chanjo ya Uviko-19.
"Pamoja na kwamba chanjo ni hiyari, lakini wanajeshi wetu wakitaka kwenda nchi fulani ni lazima wachanjwe hivyo tumeendelea kutoa elimu na kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kupata chanjo ili kujikinga na Uviko-19," amesema
Naye Kaimu Mkuu wa chuo hicho cha Kijeshi Lugalo, Luteni Kanali Sisco Kalongola amesema chuo hicho kimekuwa kikishirikiana na Serikali pamoja na hospitali ya Jeshi katika kutoa elimu na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo ya Uviko-19.
"Tangu tukiwa wadogo tulikuwa tunachanjwa kwa nini tuogope kuchanjwa sasa hivi, tuqche kusikiliza stori za mitaani tujitokeze kwa wingi kupata chanjo," amesema
Aidha amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1982 chini ya Hospitali kuu ya Jeshi na mwaka 2015 kilijitenga na kuwa chuo kamili na kuitwa Chuo cha Kijeshi cha Sayansi za Tiba.
"Tangu kuanzishwa kwake kimekuwa kikifundisha kozi za uongozi kwa maofisa katika fani za tiba, kozi za madaraja ya kijeshi katika fani za tiba, stashahada ya ofisa tabibu na stashahada ya ofisa uuguzi na ukunga," amesema
Amesema kwa mwaka huu wa masomo chuo kimefanikiwa kutunukiwa tuzo ya utendaji bora kwa kufikia daraja la kwanza la utendaji, mazingira, mafunzo na ufundishaji hivyo kuwa kati ya vyuo viwili bora vya afya nchini.