Wanakijiji wafunga barabara wakitaka iwekewe matuta

Muktasari:
- Wananchi wa Kijiji cha Wiri wilayani hapa mkoani Kilimanjaro, wamefunga barabara kwa saa kadhaa wa wakishinikiza kuwekwa matuta katika eneo hilo, baada ya mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya msingi Gararagua kugongwa na gari na kufariki dunia eneo la Datchcorner lililopo barabara ya Sanya Juu.
Siha. Wananchi wa Kijiji cha Wiri wilayani hapa mkoani Kilimanjaro, wamefunga barabara kwa saa kadhaa wa wakishinikiza kuwekwa matuta katika eneo hilo, baada ya mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya msingi Gararagua kugongwa na gari na kufariki dunia eneo la Datchcorner lililopo barabara ya Sanya Juu.
Wananchi hao wameweka matuta ya muda mfupi, huku wakitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka katika eneo hilo ili kuepusha ajali za mara kwa mara.
Mmoja wa wakazi hao, Jemes Urio amesema tangu barabara hiyo iwekewe lami magari yamekuwa yakiendeshwa kwa kasi bila kuzingatia usalama wa watumia barabara wakiwemo watembea kwa miguu.
"Katika eneo hili Tanroads wameweka matuta madogo kwa lengo la magari kupunguza mwendo, lakini badala ya kupunguza mwendo wamekuwa wakiongeza mwendo na kusababisha ajali kama hii ya mwanafunzi kugongwa na kufariki dunia.
“Tunaweka matuta makubwa ya kienyeji hata kama ni kinyume na utaratibu lakini ni kulinda usalama wa Wananchi, hadi hapo mamlaka husika watakapofika na kuweka matuta," amesema.
Amesema mbali na ajali hiyo, mwanafunzi mwingine aligongwa Januari mwaka huu katika eneo hilo, huku pia zikitokea ajali nyingine zilizosababisha vifo vya watu wanne.
“Tanroads wafike hapa na tumeweka matuta ya dharura ya kienyeji ili kudhibiti mwendo kasi," ameongeza Urio.
Kwa upande wa kijiji hicho, Hamza Munis amemuomba Meneja wa Tanroads kufika katika eneo hilo na kuweka matuta, ili kupunguza amatukio ya ajali ambayo yamekuwa yakitokea.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Thomas Apson, amesema hatasita kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaoendesha Magari bila kufuata sheria za usalama barabarani.
"Nawaomba Wananchi kuwa wapole wakati nikiwasiliana na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, kufika katika eneo hilo kuweka matuta ili kusaidia kupunguza ajali, pamoja na hayo tutawashughulikia Madereva wazembe," amesema Apson.