Wanakijiji wahofia magonjwa, kubomoka bwawa Mwadui

Muktasari:
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sofia Mjema, kufuatia kupasuaka kwa bwawa hilo linalomikiliwa na mgodi wa almasi wa Williamson Diamond, nyumba ambazo zimezingirwa na tope ni 13 na wananchi walioathirika ni 59 na watoto watatu walipata shida ya homa ya kutapika na wanaendelea na matibabu.
Kishapu. Wananchi wa kijiji cha Ng’wan’holo kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, wamesema wanahofia kukumbwa na magonjwa kutokana na tope linalotiririka kutoka katika bwawa la mgodi wa mgodi wa almasi unaomilikiwa na kampuni ya Williamson Diamond lililobomoka.
Kutokea kwa tukio hilo wameiomba Serikali iwasaidie kwa haraka ili kuepukana na tope hilo lililozingira makazi yao.
Mwananchi limeshuhudia matope hayo yakiwa yamesambaa kwenye mashamba na makazi ya wat, ambapo baadhi ya wananchi wameomba Serikali kuchukua hatua za haraka.
"Hali ya hapa kwa sasa inatatanisha na tukiendelea kukaa hapa inaweza kusababisha vifo. Mpaka sasa ninavyoongea na wewe, sijui nakwenda kulala wapi na watoto wangu.
“Nina familia ya watoto watano ila pakushika sina kabisa viongozi tumewaona wamepita tu hawajatoa msaada wowote," amesema Ester Thomas mkazi wa kijiji hicho.
Kwa upande wake Joseph Kwilasa mkazi wa kijiji hicho, amesema wanaiomba Serikali iwaokoe kwani mifugo yao imekwenda na maji baadhi ya nyumba zimebomoka na kuanguka kabisa kuna pikipiki zimefunikwa na tope hilo.
“Bwawa la maji tulilokuwa tukilitegemea nalo limeingiliwa na maji ya kutoka mgodini ambayo inawezekana si salama kwa binadamu,” amesema.
Maelezo hayo yameungwa mkono na Mipawa Dotto ambaye ni kamanda wa Sungusungu kijijini hapo akisema, “Hapa tulipo hatuna maji ya kunywa wala ya kutumia kwa sababu bwawa letu limeharibika kwa kuingiliwa na maji yasiyo salama.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Manai, Ester Seni, amesema wanaiomba Serikali kufanya tathimini ya athari ambazo wamezipata wananchi, na waone namna ya kuwasaidia.
“Tunaomba wataalam kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini tope hilo kama linaweza kuleta madhara kwa wananchi, sababu limetoka ndani ya mgodi huenda kuna sumumm” amesema.
Awali, Mkuu wa Mkoa, Sophia Mjema akizungumzia suala hilo jana mchana, amesema Serikali ipo bega kwa bega kuwasaidia wananchi walioathirika na janga hilo na kwamba mgodi tayari umechukua jukumu la kuwapelekea chakula na maji.
"Mpaka sasa nyumba ambazo zimezingirwa na tope ni 13, na wananchi walioathirika ni 59 na Kaya 19 na watoto watatu walipata shida ya homa ya kutapika na wanaendelea na matibabu.
“Serikali tumeshaunda kamati itakayochunguza tukio hilo na itakuja na majibu yote pamoja na kutoa tathimini ya ujumla,” amesema Mjema.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetuma wataalamu wake kwenda kukagua bwawa la maji yenye kemikali katika Mgodi wa Mwadui mkoani Shinyanga.
Wakati NEMC ikitangaza hatua hizo, tayari kampuni ya Petra Diamonds inayomiliki mgodi huo imesitisha uchimbaji huku maji yanayovuja yakijaa katika mitaa jirani.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka amesema tayari wataalamu hao wameshawasili Mwadui kutathmini ukubwa wa athari zilizojitokeza.
“Tunakusudia kuzuia mafuriko zaidi mtaani ambayo yameenea katika eneo la kilomita nane. Tunajitahidi kuzuia kusambaa zaidi kwa matope na uchafu mwingine kutoka mgodini,” alisema Dk Gwamaka.
Mgodi wa Mwadui unamilikiwa kwa ubia wa Serikali yenye asilimia 25 na kampuni ya Patra Diamonds yenye asilimia 75.