Wananchi wafunga barabara wakitaka ikarabatiwe

Barabara ya Lukobe- Mazimbu ikiwa imefumgwa na wananchi baada ya kushindwa kupitika na kusababisha nauli kupanda. Picha na Johnson James
Muktasari:
- Wananchi wa Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro, wameitaka Wakala wa Barabara za Vijijni (Tarura) kuitengeneza kwa dharura barabara ya kata hiyo ili kurahisisha usafiri katika eneo hilo.
Morogoro. Wananchi wa Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro jana Ijumaa Juni 7, 2024 wamefunga barabara ya Lukobe mwisho mpaka Mazimbu wakilalamikia ubovu wake unaosababisha wasifikiwe na usafiri.
Mwananchi Digital imeshuhudia baadhi ya wakazi wa Lukobe wakiwa wamekusanyika na wakitoa kauli za kuitaka Wakala wa Barabara za Vijijni (Tarura) kuitengeneza kwa dharura barabara hiyo.
Hassan Seleman amesema kwa muda mrefu wakazi wa Lukobe wamekuwa wakipata changamoto za kufika kwenye maeneo yao ya kufanya shughuli za kiuchumi, sababu ya barabara kuwa mbovu jambo linalosababisha hata daladala kushindwa kufika kwenye maeneo yao.
"Barabara hii ya Lukobe mwisho kuelekea Mazimbu Road, tumeifunga baada ya kuwa mbaya kiasi cha baadhi ya maeneo kutofikika kwa urahisi. Kutokana na hali hii nauli ya kutoka hapa Lukobe kwenda mjini tunalazimika kutumia nauli hadi Sh4,000 kwenda na kurudi kwa kutumia bajaji wakati nauli ya kawaida ni Sh1,400.
"Umefika wakati watoto wetu wanatembea umbali mrefu kwenda shule maana kwa sasa hakuna daladala kutokana na ubovu wa barabara, huduma za maji zimepanda awali dumu moja tulikua tunapata kwa Sh500 lakini kwa sasa dumu moja tunauziwa Sh800," amesema Seleman.
Kwa upande wake, Ramadhan Mohamed amesema kuwa ubovu wa barabara hiyo umekuwa kero jambo ambalo Serikali inatakiwa kuwasaidia kupata suluhisho maana hali ni mbaya
"Kutokana na ubovu huu, daladala zilizokuwa zinakuja hapa Lukobe kwa sasa hazifiki na badala yake tunatumia usafiri wa bajaji ambao umekuwa na gharama kubwa tunataka, Tarura warekebishe barabara hii," amesema.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma amefika eneo hilo na kuiagiza Tarura wilayani hapa kukarabati barabara hiyo ndani ya muda mfupi
"Hatuwezi kuwa na barabara mbovu namna hii kwenye manispaa yetu, wananchi hawa wameamua kufanya hivi baada ya kukosa haki zao za msingi hivyo Tarura nawaelekeza kuijenga hii barabara ndani ya muda mfupi," amesema.
Alipotafutwa Meneja wa Tarura Wilaya ya Morogoro, Mohamed Mwanda amesema wameshapata zaidi ya Sh300 milioni kwa ajili ya kutengeneza barabara hiyo.
"Kwa muda mfupi ujao mkandarasi ataingia kazini kuhakikisha barabara inapitika ndani ya muda mfupi ili wananchi waendelee kupata huduma zao kama kawaida," amesema Mwanda.