Wananchi wapata hofu kukosekana dawa kutibu sumu ya nyoka

Muktasari:
- Ukosefu wa dawa za nyoka (sindano) katika Zahanati za Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kumetajwa kuwa mwiba ambao unasababisha watu wanaong’atwa na nyoka kufariki huku zikitolewa kwa bei ya juu ambapo kwa sindano moja ni zaidi ya Sh200,000.
Mtwara. Ukosefu wa dawa za nyoka (sindano) katika Zahanati za Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kumetajwa kuwa mwiba ambao unasababisha watu wanaong’atwa na nyoka kufariki kutokana na kukosa matibabu.
Akizungumza na Mwananchi, Diwani Viti Maalum wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Mariam Lilepe amesema kuwa ili kunusuru maisha ya wananchi walio wengi wenye kipato kidogo Serikali inapaswa kugharamia matibabu ya wananchi walioumwa na nyoka bure.
“Tunaiomba Serikali itupunguzie bei ya hizo dawa hasa ukizingatia kuwa tatizo hili limekuwa likigharimu maisha ya watanzania msitoe dawa kwa kuridhisha mtu toeni dawa ziwasaidie wananchi,”amesema Lilepe.
Diwani wa Kata ya Nalingu, Said Ally Amri amesema kuwa licha ya kufikisha maombi hayo mara kwa mara ya kusogezewa dawa hizo katika zahanati zilizopo karibu na watu lakini utelezaji umekuwa hafifu.
“Nyoka hawezi kukungata ukachukua hata nusu saa ukiwa hai wapo waliopoteza maisha baada ya kung’atwa na nyoka kutokana na kuchelewa kupata matibabu,” amesema Amri.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nalingu, Mohamed Naivalula amesema kuwa dawa hazipo zahanati licha ya watu wengi kupatwa na tatizo hilo lakini bado hatua stahiki za kusogeza huduma hazijachukuliwa.
“Isitoshe dawa zikiwepo ni ghali sana tunanunua zaidi ya shilingi laki mbili na ikumbukwe kuwa nyoka huuma kwa dharula huwezi tunza fedha ukisubiri kuumwa na nyoka na ukienda kituo cha afya unaambiwa mpaka utoe fedha ndio upate matibabu,” amesema Naivalula.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Selemani Nampanye amekiri kuwa halmashauri hiyo ina uhaba wa dawa dawa za nyoka ambapo hupatikana kwa uchache.
“Kuna wakati dawa zilikuwepo ila zimeisha tumeomba ziletwe tena na safari hii ziende moja kwa moja kati Zahanati za Msangamkuu, Ziwani, Nalingu, Madimba, Tangazo, Kilambo, Kitere, Naumbu na Mayanga maeneo yenye athari kubwa,” amesema.
“Mfano mtu akiumwa na nyoka Nalingu ili awahi Kituo cha Afya Nanguruwe anatakiwa kwenda umbali wa kilomita 15 hawezi kutoboa kwanza angalia umbali wenyewe alafu kumbuka sumu pia inasambaa mwilini,” amesema.
“Ni vyema wanachi wapewe elimu mtu akiumwa na nyoka nini kifanyike mara baada ya kuumwa ukitembea zaidi ya dakika tano bora ukae zaidi ya dakika ishirini ukisubiri matibabu,” amesema Nampanye.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Joel Tiho anasema kuwa wameshachukua hatua za dharula kwakusambaza dawa hizo katika baadhi ya zahanati na vituo vya afya ambavyo kumeonekana kuwepo kwa changamoto ya watu kuumwa na nyoka.