Wanandoa Mafinga wapewa neno kudumisha ndoa zao

Muktasari:

 Ndoa nyingine zimevunjika chanzo kikiwa umasikini kwa sababu wanawake wanapoolewa wanadhani watakuwa wamepata suluhisho katika maisha yao


Mufindi. Wanandoa katika Halmashauri ya Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wameshauriwa kutatua migogoro katika ndoa zao ili waweze kuishi vizuri na familia zao.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake leo Januari 11, 2024, Ofisa Ustawi wa jamii katika halmashauri hiyo, Swanah Sudi amesema ni vema wazazi wakaishi pamoja kwa ajili ya kuwalea watoto wao ili waweze kukua katika maadili mema.

Amesema familia nyingi zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya migogoro ya ndoa, hali ambayo imesababisha ndoa nyingi kuvunjika kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo.

“Uvumilivu unatakiwa katika ndoa, sio ikitokea changamoto kidogo tu kwenye familia basi wazazi wanakimbia kudai talaka kwa sababu wakifanya hivyo waathirika wakubwa wanakuwa ni watoto,” amesema Sudi.

Sudi ametaja madhara ambayo watoto wanaweza kupata baada ya wazazi wao kuachana ni kukosa haki zao za misingi ikiwemo chakula, mavazi yanakuwa shida kwao pamoja na uvunjifu wa haki za watoto.

Msaidizi wa kisheria wa shirika lisilo la kiserikali Mafinga (LREO), Jimmy Mgavano amesema mfumo wa maisha ndio chanzo cha wanawake wengi kudai talaka kutokana wengi wao kuingia kwenye uhusiano bila kuchunguzana.

“Kwa sasa kumekuwepo na ongezeko la wanawake kudai talaka, sisi kama LREO tumepokea kesi tano ambazo wote wamechukua talaka zao lakini madai yao ya kutaka talaka ni kwamba waume zao kutaka kuwaua kwa sababu ambazo hazijulikani,” amesema Mgovano.

Amesema ndoa zingine zimevunjika chanzo kikubwa kikiwa umasikini kwa sababu wanawake wanapoolewa wanadhani watakuwa wamepata suluhisho katika maisha yao.