Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanawake wahimizwa kugombea uchaguzi wa serikali za mitaa

Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika kimkoa Wilayani Bukombe

Muktasari:

  • Wito huo umetokana na ukweli kuwa wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa idadi ndogo katika chaguzi zilizopita.

Geita. Wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024, wanawake wametaakiwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali na kutoogopa vitisho vya wanaume.

Wito huo wa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed umekuja kutokana na idadi ndogo ya wanawake ambao wamekuwa wakijitokeza katika chaguzi zilizopita.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Nchi, ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, wanawake waliogombea walikuwa asilimia 33 ya wagombea wote.

Sakina ametoa wito huo wakati wa maadhimisho ya wiki ya elimu ya watu wazima, yaliyofanyika kimkoa wilayani Bukombe akisisitiza kwamba uchaguzi ni fursa kama zilivyo nyingine, hivyo wanawake wasikubali kubaki nyuma.

Mkuu huyo wa wilaya amesema wanawake wanapata hofu ya kujitokeza kugombea wakiogopa kutishwa na wanaume na hivyo akawataka kutokubali vitisho, wajitokeze kwa wingi kugombea.

Amesema ile dhana ya 50 kwa 50 wanayotaka kuifikiwa inahusisha matumizi ya akili kwa kuwa Mungu ameweka akili sawa kwa mwanaume na mwanamke, hivyo ni fursa kwao kuchukua fomu na kuingia kwenye ushindani.

“Nitumie fursa hii kuwasihi mjitokeze kujiandikisha kwa wingi kuchagua viongozi wastahimilivu, wenye ueledi wa kutosha na zaidi nawaomba sana mjitokeze kuchukua fomu mgombee nafasi zitakazotangazwa,” amesema Sakina.

Amesema badala ya kubaki nyuma na kusubiri uchaguzi upite kisha kuanza kuilalamikia Serikali, ni vema watumie fursa hiyo kuchukua fomu na kuingia kwenye kinyang’anyiro ili kuleta mabadiliko chanya.

“Tunyanyuke tukachukue fomu tuepuke kuchagua viongozi wasiokubalika, wanaotumia uongozi wao vibaya. Hakuna kura za bure, kila mmoja ahakikishe kabla ya kuchukua fomu anakubalika kwa wananchi,” amesema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Vyama vya Siasa mkoani Geita, Ikorongo Otto amesema katika baadhi ya maeneo, wanawake wanakutana na mitazamo ya kijamii inayowazuia kutoka nyumbani kwa shughuli za siasa.

Scolastica Mashauri, mkazi wa Bomani, mjini Geita amesema changamoto ya rasilimali fedha ni moja ya sababu zinazowakwamisha kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kwenye chaguzi mbalimbali.

“Kugombea nafasi za kisiasa kunahitaji rasilimali za kifedha na usaidizi wa kiutawala. Wanawake wengi wanakosa uwezo wa kifedha ukikutana na wajumbe tayari wamejengewa mazingira ya kupokea, wewe huna kipato huwezi kuwashawishi,” amesema.

Kwa upande wake, Salma Mrisho, mwandishi wa habari mkoani Geita, amesema jamii nyingi bado zina mitazamo ya kijinsia ambayo inaweza kuwafanya wanawake wahisi kuwa si sehemu ya shughuli za siasa.

Amesema wanawake wanaweza kujihisi kuwa siyo jukumu lao kuongoza, au kuhofia kukataliwa na jamii zao na hiyo inatokana na elimu ndogo na uelewa mdogo wa haki zao:

“Jambo jingine ni umaskini na changamoto za kiuchumi, hizi zinaweza kuwafanya wanawake washindwe kugharamia kampeni za kisiasa au kushiriki kikamilifu katika uchaguzi, lakini pia  kudhalilishwa kwa sababu ya jinsia zao vinawafanya wasijitokeze ili wawe salama,” amesema Mrisho.


Nini kifanyike

Ili kuhamasisha wanawake wanajitokeza kugombea, Serikali na wadau mbalimbali wametakiwa kutoa elimu na taarifa kuhusu haki na fursa za wanawake katika siasa ili kuondoa vikwazo vya kijamii na kuongeza ufahamu.

“Wanawake wana nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko chanya katika jamii zetu. Tunahitaji kuona wanawake wengi wakijitokeza kugombea na kuchangia katika uongozi na penye kiongozi mwanamke huwezi kukuta pana ufisadi kwa kuwa wao ndani yao wameumbiwa nidhamu na hofu,” amesema Otto.

Amesema Serikali na vyama vya siasa wanapaswa kuweka sheria na sera za kulinda wanawake dhidi ya unyanyasaji wa kisiasa na kijinsia ili kuwafanya wajisikie salama kushiriki kukuza usawa wa kijinsia katika vyama vya siasa.