Wanawake wenye fistula watakiwa kujitokeza kutibiwa

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Saidi Mtanda akipata maelezo kutoka kwa wataalam wa afya kutoka kituo cha Afya cha Kivulini Maternity Center, katika maadhimisho ya Kimataifa ya kutokomeza ugonjwa wa fistula,leo jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

Kwa mujibu wa utafiti wa shirika la chakula duniani (UNFPA) uliofanyika nchini Tanzania, wanawake kati ya 10,000 hadi 20,000 na kila mwaka kuna wagonjwa wapya kati ya 3,000 ambapo 1,300 pekee ndiyo hupata matibabu.

Arusha. Wanawake wenye matatizo ya ugonjwa wa fistula mkoani Arusha wametakiwa kuondoa aibu na kuacha tabia ya kujifungia ndani na badala yake kwenda kupata matibabu.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 23, 2022 na mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ugonjwa wa fistula yaliyoandaliwa na kituo cha afya cha Kivulini Maternity Center cha jijini Arusha.

Amesema kwa mujibu wa utafiti wa shirika la chakula duniani (UNFPA) uliofanyika nchini Tanzania, wanawake kati ya 10,000 hadi 20,000 na kila mwaka kuna wagonjwa wapya kati ya 3,000 ambapo 1,300 pekee ndiyo hupata matibabu.

"Tatizo la fistula lipo lakini ipo dhana ya jamii kuwaficha na kutotaka kueleza kwamba tatizo la fistula lipo, hata wagonjwa wenyewe wa fistula wanajificha wakidhani kupata ugonjwa fistula ni fedheha au aibu.

"Tunasisitiza kama serikali wale wote ambao wana ugonjwa huo ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine, hakuna aibu wahini kwenye vituo vya kutoa huduma na matibabu yake ni bure. Hakuna gharama tunashukuru Fistula Foundation kwa kuendelea kufadhili mashirika mbalimbali ili yaweze kupambana na ugonjwa wa fistula, tunawapongeza Maternity Africa," amesema Mtanda.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka kituo hicho cha Kivulini, Dk Fredrick Mbise, amesema wanaendelea kusisitiza jamii ikiwemo wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki mapema na kujifungulia katika vituo vya afya ili kupata matibabu haraka pindi wanapopata tatizo hilo.

Ametaja baadhi ya sababu zinazochangia wanawake kupata fistula ni pamoja na changamoto ya  miundombinu pamoja na baadhi ya wanawake kujifungulia nyumbani kwa sababu mbalimbali ikiwemo umbali wa vituo vya afya.

"Wengi wanaopata tatizo hilo ni wale wanaojifungulia nyumbani,wengine ni wale wanaojifungulia njiani kutokana na changamoto ya umbali wa kufuata huduma za afya," amesema.

"Fistula ambayo siyo ya uzazi inatokana na saratani ya shingo ya kizazi,hivyo tuanendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kufanya vipimo mara kwa mara na kuepukana na ugonjwa huo,huku nyingine ikichangiwa na upasuaji ambao unahatarisha kuumia kwa kibofu au njia ya mkojo,"

Mmoja wa wakazi wa jiji la Arusha ambaye alishawahi kuugua ugonjwa huo, Ester Steven amesema alipata tatizo hilo mwaka 2007 alipokuwa akijifungua mtoto wa nne na kuwa aliteseka na ugonjwa huo kwa kipindi cha miaka saba kabla ya kupatiwa matibabu.

"Nimeteseka sana kwa kipindi cha miaka saba, kwani nilikuwa natokwa na haja kubwa na ndogo kwa wakati mmoja, mume alinivumilia ikafika mahali akaniacha, nilikuwa nakaa ndani tu maana ile hali unatakiwa ujifanyie usafi kila mara.

"Ila baada ya kupatiwa matibabu kituo cha Kivulini nashukuru nimepona na sasa ninaendelea vizuri. Nawasihi wanawake wenzangu wenye tatizo kama hilo wasijifiche ndani watoke linatibika na matibabu ni bure kabisa," amesema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa halmashauri ya Arusha, Dk Petro Mboya amesema idadi ya wagonjwa wa tatizo hilo imepungua kwa kiasi kikubwa mkoani Arusha kutokana na akina mama wenye tatizo hilo kujitokeza na kupatiwa matibabu kituoni hapo.

Naye Ruth Mollel kutoka katika kituo hicho, amesema tangu kuanza kituo hicho mwaka 2018 wameweza kuwatibu wanawake zaidi ya 450 waliokuwa na tatizo la fistula,huku wanawake waliojifungua katika kituo hicho wakiwa zaidi ya 8000.