Wanne washikiliwa na Polisi Dar kwa kutishia watu na bastola

Wednesday August 04 2021
ashikiliwapic
By Tatu Mohamed

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kutishia watu silaha wanazozimiliki kihalali.

Watuhumiwa hao ni Isack Robert Wile Wambura, (44) ambaye ni mkazi wa Sinza E, Rashid Iddi Mshana (36), mkazi wa Mwenge, Mussa Rashid Mshana (39) ambaye ni mkazi wa Mwenge na Ibrahim Shaibu, (52) ambaye ni mkazi wa Kinyerezi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 4, 2021 Kamanda wa polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema mtuhumiwa wa kwanza, Wambura akiwa katika baa iitwayo 99 Vibes iliyopo Sinza alitoa silaha yake bastola aina ya Browning yenye namba TZCAR 72791 na kuanza kutishia watu huku akiwa amelewa pombe.

Mtuhumiwa wa pili, Rashid Iddi Mshana alionekana kwenye video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii akitishia kwa silaha bastola aina ya Browning

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam lilifanya upelelezi na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na silaha bastola yenye namba AP 06929TZCAR 113729 ikiwa na risasi 10 ndani ya magazine inayomilikwa na kaka yake anayefahamika kwa jina la Mussa Rashid Mshana," amesema.

Amemtaja mtuhumiwa wa tatu, Mussa Rashid Mshana anayetuhumiwa kwa kosa la uzembe la kumuachia silaha mdogo wake ambaye ni Rashid Iddi Mshana.

Advertisement

Mdogo wake huyo alijirekodi akitishia watu  silaha hiyo na  kutuma video kwenye mitandao ya kijamii.

"Mtuhumiwa wa nne, Ibrahim Shaibu Agosti 1, 2021 majira ya saa 12:00 jioni maeneo ya Vijibweni Kigamboni alimtishia kumuua kwa silaha jirani yake aliyefahamika kwa jina Chacha Mwita walipokuwa wanagombania mipaka ya kiwanja katika maeneo yao," amesema.

Aidha ametoa onyo kwa ambao wanatumia silaha ovyo na kusema kuwa hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao.


Advertisement