Waomba sheria ya watu wenye ulemavu mwaka 2004 ifanyiwe marekebisho
Arusha. Wadau kutoka sekta ya umma na binafsi wameshauriwa kuboresha huduma za afya kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kujenga miundombinu ya kutosha katika vituo mbalimbali vya afya pamoja na kuwepo kwa wataalamu wa kutosha katika kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu hususani viziwi.
Hayo yalisemwa mkoani Arusha na mtoa mada katika mafunzo ya Shirika linalojihusisha na Maendeleo ya Vijana katika nyanja za Afya, Uchumi na Uongozi (DSW), Dk Fredrick Msigallah wakati akizungumza kwenye semina kuhusu afya ya uzazi kwa waandishi wa habari na maafisa habari iliyofanyika mkoani hapa na kuandaliwa na Shirika la DSW.
Msigallah alisema sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 imepitwa na wakati hivyo inatakiwa ifanyiwe mapitio iendane na wakati kwa kuzingatia mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu wa mwaka 2006.
Alisema watu wenye ulemavu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kupata huduma jambo ambalo huwakwamisha na wengi wao kuishia kukata tamaa.
"Tunaomba pia vyuo vya uuguzi viweke kozi za utoaji huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwemo mafunzo ya lugha ya alama iwe sehemu ya mitaala yao ili wataalamu wanaomaliza wawe na ujuzi wa kutosha katika kutoa huduma kwa jamii ya watu wenye ulemavu hususani viziwi," alisema
Kwa upande wake Meneja Uraghibishi na Mahusiano kutoka DSW, Philomena Marijani alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wadau hao kuhusu afya ya uzazi katika jamii pamoja na huduma jumuishi ya afya na jinsia kwa watu wanaoishi na ulemavu.
Philomena alisema wamekuwa wakishiriki na kuangalia namna ya kuwasaidia watu wa makundi maalumu katika kujikwamua kiuchumi na kuweza kuondokana na changamoto mbalimbali.
"Kuna haja kubwa sana ya kuwepo kwa wataalamu wa lugha za alama katika vituo vya afya ili kurahisisha huduma za afya kwa watu wenye ulemavu kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi sana wakati wa kufuata huduma hizo na kushindwa kutatua changamoto zao kwa wakati," alisema.
Mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Viziwi na Jamii (DCPO), Ramadhani Hamisi alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa katika kupata huduma za afya kutokana na kutokuwepo kwa wataalamu wa lugha za alama hali ambayo inachangia wengi wao kukosa huduma na kuendelea kuteseka.
"Kuwepo kwa wataalamu wa lugha za alama ndani ya hospitali kutasaidia sana kwetu sisi kupata huduma rafiki na sahihi ndani ya jamii kwani wengi wa walemavu wamekuwa wakiendelea kuteseka kutokana na kukosekana kwa wataalamu hao hivyo naomba sana serikali itusaidie katika hilo," alisema