Wasiwasi majitaka ya mgodini yakisambaa katika makazi ya watu

Muktasari:
Wakati Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) likiendelea kuzuia majitaka yenye tope yanayotoka katika mgodi wa Williamson Diamond kuingia kwenye makazi ya watu, wataalamu wa madini wameonya wananchi kutoyasogelea hadi watakapopewa taarifa yapo salama.
Dar/Kishapu. Wakati Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) likiendelea kuzuia majitaka yenye tope yanayotoka katika mgodi wa Williamson Diamond kuingia kwenye makazi ya watu, wataalamu wa madini wameonya wananchi kutoyasogelea hadi watakapopewa taarifa yapo salama.
Maji hayo ambayo NEMC inaendelea kuyadhibiti, yametokana na bwawa la majitaka la mgodi huo unaomilikiwa na kampuni hiyo (asilimia 75) na Serikali (asilimia 25) kupasuka majuzi na kutiririsha maji hayo yenye tope kwenye makazi ya watu.
Jana Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samwel Gwamaka akizungumza na Mwananchi kwa simu alisema kazi kubwa inayoendelea Mwadui ni kuzuia tope hilo lisiendelee kusambaa.
Akitoa tahadhari kwa wananchi, Mtaalamu wa Madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Karim Baruti alisema kama kuna mito katika maeneo ambayo tope hilo linatiririka, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari.
“Ni lazima tujue hayo maji yakitoka yanaelekea wapi, yatakuwa na athari kwenye eneo kubwa au dogo, lakini wananchi hawapaswi kuyasogelea au kuyatumia mpaka watakapoambiwa ni salama au sio salama,” alisema.
Mtaalamu mwingine wa madini ambaye hakutaka jina litajwe aliwatupia mzigo NEMC na kampuni husika akisema ndio wenye jukumu kisheria la kujua maji ya mgodini yanayotumika kuchenjua madini yametibiwa kwa kiwango cha kutokuwa na madhara.
Alieleza hatua za uchenjuaji wa madini kutokana na aina ya uwekezaji uliofanyika, ukiwemo ule ambao huhusisha kemikali ambazo huwa ni sumu.
“Mara nyingi sheria zetu za nchi zinaainisha kwamba mtu anayefanya kazi fulani lazima maji aliyotumia kwenye uchenjuaji ayatibu ndipo ayaweke kwenye mabwawa,” alieleza.
Mtaalamu huyo alisema upo utaratibu mwingine wa uchenjuaji ambao unahusisha maji pekee, lakini hatari yake ni tope ambalo hutokea wakati wa uchenjuaji, ambalo pia ni hatari linapoingia kwenye makazi ya watu, hasa kwa kusababisha uharibifu wa miundombinu.
Kwa mujibu wa mtandao wa Quora, kemikali zinazotumika kuchenjua almasi ni pamoja na tindikali ya sulphuric, alcohol, hydrogen peroxide na acetone.
Pia mtandao wa Free Patents Online unaitaja sulfuric acid kuwa kiungo muhimu katika uchenjuaji wa almasi.
Waiangukia Serikali
Wakazi wa Kijiji cha Ng’wan’holo, Kata ya Mwadui Lohumbo wameeleza hofu yao ya kukumbwa na maradhi kutokana na maji yenye tope yanayotiririka kutoka katika mgodi huo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema aliyezungumzia suala hilo juzi, tayari nyumba ambazo zimezingirwa na tope hili ni 13 na wananchi walioathirika ni 59 na watoto watatu walipata shida ya homa ya kutapika na wanaendelea na matibabu.
Taarifa zilizopatikana katika mtandao wa Advancing Earth and Space Science, zinasema bwawa hilo limebomoka ukuta wake wa mashariki.
Kutokea kwa tukio hilo, wananchi katika kijiji hicho wameiomba Serikali iwasaidie kwa haraka ili kuepukana na maji hayo, kwa kuwa maji hayo yameingia pia katika bwawa lenye maji wanayotumia kupikia na kunywa.
“Hali ya hapa kwa sasa inatatanisha na tukiendelea kukaa hapa inaweza kusababisha vifo. Mpaka sasa ninavyoongea na wewe, sijui nakwenda kulala wapi na watoto wangu.
“Nina familia ya watoto watano ila pakushika sina kabisa, viongozi tumewaona wamepita tu hawajatoa msaada wowote,” alisema Ester Thomas, mkazi wa kijiji hicho.
Kwa upande wake Joseph Kwilasa, pia mkazi wa kijiji hicho alisema wanaiomba Serikali iwaokoe kwani mifugo yao imesombwa na maji hayo yalipotoka kwa kasi, baadhi ya nyumba zimebomoka na kuanguka na kuna pikipiki zimefunikwa na tope hilo.
“Bwawa la maji tulilokuwa tukilitegemea nalo limeingiliwa na maji ya kutoka mgodini ambayo inawezekana si salama kwa binadamu,” alisema.
Maelezo hayo yameungwa mkono na Mipawa Dotto, ambaye ni Kamanda wa Sungusungu kijijini hapo akisema, “hapa tulipo hatuna maji ya kunywa wala ya kutumia majumbani kwa sababu bwawa letu limeharibika kwa kuingiliwa na maji yasiyo salama.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Manai, Ester Seni ameiomba Serikali kufanya tathimini ya athari ambazo wamezipata wananchi na ione namna ya kuwasaidia.
Akizungumzia uharibifu na mali zilizopotea, Diwani wa Kata ya Mwadui, Lohumbo Manyanda anasema kuna watu wamedai wamepoteza kuku na mbuzi, lakini mpaka sasa idadi ya mifugo hiyo haijajulikana, wanaendelea na tathimini watatoa taarifa baadaye.
“Wale ambao nyumba zao ziliathiriwa na maji tumewahifadhi shuleni, baadaye watapelekwa Mwadui.
Hata hivyo, alisema mpaka juzi hakuna mfugo ulioonekana umedondoka kwa sababu ya maji hayo na Serikali inaendelea na uchunguzi wa maji hayo ili kujua kama yana madhara kwa binadamu.
Diwani mwingine wa Kata ya Kishapu, Joel Ndetoson alisema maji hayo yamefika Mto Tungu.
“Maji haya yalifika huku usiku baada ya mvua kunyesha, naona kwa sasa yatakuwa yamefika Kata ya Mwamashele sababu yanatembea, hivyo tumepiga marufuku wananchi wasitumie maji hayo na wasinyweshe mifugo yao, badala yake baadhi wanachimba ya ardhini na wengine wanatumia ya Ziwa Victoria,” alisema Ndetoson.
Diwani wa Kata ya Igaga wilayani Kishapu, James Kamuga alisema hali ni mbaya, watu waliokuwa wanafuata maji mtoni wamepigwa marufuku kwa sababu maji hayo hayaaminiki tena.
Taarifa ya Petra Diamond, kampuni tanzu inayomiliki mgodi huo iliyotolewa katika mtandao wa Miningmx imesema kwa sasa uzalishaji umesimamishwa kutokana na ajali hiyo.
“Hakuna vifo vilivyothibitishwa kutokea kutokana na kupasuka kwa bwawa hilo,” imeeleza taarifa hiyo.
Wawakilishi wa kampuni pamoja na Serikali na huduma za dharura wanaendelea kuwaweka wanavijiji mbali na eneo lililoathirika,” imesema taarifa hiyo.
Mabwawa hatari duniani
Kwa mujibu wa mtandao wa Reuters wenye ripoti ya mabwawa yaliyo hatari zaidi duniani katika mikodi ya almasi, upande wa Tanzania uko chini kabisa.
Nchi inayoongoza kwa kuwa hatarini kutokana na mabwawa hayo ni Afrika Kusini ikiwa na mabwawa hatarishi karibu 80, ikifuatiwa na Marekani yenye 40.
Nchi nyingine ni Australia, Brazili, Canada, Ghana, Mexico, Peru, Botswana ambazo zina mabwawa kati ya 37 na nne huku Tanzania ikitajwa kuwa na mabwawa chini ya manne.
Uzoefu migodi mingine
Aprili 2022 Mgodi wa Barrick North Mara uliopo mkoani Mara ulipigwa faini ya Sh1 bilioni na NEMC kwa kosa la uchafuzi wa mazingira baada ya bomba linalopitisha majitaka kutoka kwenye mgodi huo kupasuka na kutiririsha maji katika Mto Tigite.
Machi 2022 ilizuka hofu kwa baadhi ya wananchi wa vijiji vinavyopakana na Mto Mara, baada ya maji meusi kuonekana huku samaki waliokufa wakielea majini, hali iliyoelezwa ni kutokana na kukosa hewa.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) Machi 12, 2022 kulikuwepo kiwango kikubwa cha mafuta yaliyosababisha kukosekana hewa ya oksijeni kwenye maji.