Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataka kibano kwa wahusika njama za kupita bila kupingwa

Dar es Salaam. Sintofahamu ya wagombea kupita bila kupingwa huenda ikapata dawa endapo mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCONGO) kuhusu marekebisho ya sheria tano za uchaguzi yatafanyiwa kazi.

NaCONGO katika mapendekezo yake inataka kuboresha baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yanasababisha baadhi ya wagombea kupita bila kupingwa au wengine kushindwa kuwasilisha fomu zao za uteuzi na kupelekea hali hiyo wakati wa uchaguzi nchini.

Mapendekezo hayo yanalenga kurekebisha Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya gharama za uchaguzi, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya elimu ya uraia.

Sheria nyingine ni ile ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge, Madiwani na viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji.

Miongoni mwa mapendekezo yao ni kuwa ukichukua fomu ya kugombea nafasi ya kisiasa na kwa makusudi ukaacha kuirejesha ili kutoa nafasi kwa mgombea mwenzako kupita bila kupingwa, uwe hatarini kuzuiwa kugombea kwa miaka 20.

Si hivyo tu, hata kama kwa makusudi mtu huyo ameamua kutorudisha fomu, achunguzwa na ama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) au Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini iwapo uamuzi huo umeshinikizwa na rushwa.

Mapendekezo ya NaCONGO kuhusu maboresho ya sheria hizo, ni muitikio wa barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliyoiandika kwa vyama vya siasa na mashirika hayo, akitoa siku 10 za kutoa mapendekezo.

Haja ya marekebisho ya sheria hizo, inatokana na malalamiko ya muda mrefu ya wanasiasa na wadau kuhusu kutokuwepo kwa haki na uhuru katika uchaguzi unaofanyika nchini.

Hata hivyo, licha ya maboresho ya sheria hizo ambayo mchakato unaendelea, wapo wanaopendekeza iwepo tume huru ya uchaguzi yatatokana na kuundwa kwa Katiba Mpya.

Miongoni mwa maeneo yanayolalamikiwa katika sheria za sasa ni hilo la wagombea kupita bila kupingwa hasa katika mazingira yenye utata

Uchaguzi ambao wagombea wengi walipita bila kupingwa ni wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020; huku wagombea wengi wa vyama vya upinzani wakienguliwa kwa madai ya kutokidhi vigezo.

Katika chaguzi hizo, chama tawala CCM kilishinda kwa asilimia zaidi ya 90.


Mapendekezo yenyewe

Kuhusu sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge, madiwani na viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji, baraza hilo limetaka maboresho yafanyike kumzuia kugombea kwa miaka 20, yeyote atakayebainika amekusudia kutorudisha fomu ili kumpa mgombea mwenzake nafasi ya ushindi bila kupingwa.

Pia, lilitaka mgombea anayechukua fomu na kwa makusudi akaacha kuirudisha, achunguzwe na NEC na Takukuru kubaini iwapo uamuzi wake huo umesukumwa na rushwa.

Lakini, kwa ujumla baraza hilo, limesema ili kutekeleza malengo ya sheria hiyo ni vema kuondolewa kwa utaratibu wa kupita bila kupingwa na badala yake anayekosa mshindani apigiwe kura na wananchi kupata ridhaa ya kuongoza.

“Pia, sheria itamke kuwa mgombea anayefika katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi na kutomkuta, achukuliwe kuwa amewahi muda wa kurejesha fomu hata msimamizi akirudi nje ya muda,” lilipendekeza baraza hilo.

Mapendekezo mengine katika sheria hiyo ni kuwepo rukhsa ya mtu kugombea nafasi ya kisiasa bila kudhaminiwa na chama cha siasa kwa maana mgombea huru, suala ambalo limepigwa danadana muda mrefu.

“Iruhusiwe kuwa mtu yeyote anayetaka kuomba ridhaa ya Watanzania kuwaongoza, aruhusiwe kufanya hivyo ama kwa kudhaminiwa na chama cha siasa, muungano wa vyama au wadhamini huru wasiowakilisha chama cha siasa ilimradi ni wapiga kura walioandikishwa katika daftari la kudumu la mpiga kura,” limependekeza.


Sheria ya NEC

Pamoja na baraza hilo kupendekeza mabadiliko ya jina la mamlaka inayosimamia uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hadi kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, pia limetaka muundo wake ubadilike.

Kulingana na baraza hilo, muundo huo uwe na wajumbe tisa kwenye eneo la usimamizi wa tume watakaohusika na kusimamia mamlaka hiyo, huku sehemu ya pili ikiwa ni utendaji wa tume yenyewe.

Lakini, limependekeza kusiwepo chombo chochote chenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi kama inavyofanya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) badala yake jukumu hilo liachiwe NEC.

Ili kuongeza uhuru na haki kwa tume, NaCONGO imependekeza uteuzi wa wajumbe na Mkurugenzi wa NEC ufanywe na kamati itakayoundwa kwa majukumu ya kusajili wajumbe na kupendekeza majina kwa Rais.

“Kamati hii itakuwa na majukumu makubwa mawili, kusajili wajumbe wa tume, kupendekeza majina kwa Rais na wataapa mbele ya Rais ndani ya siku 30,” imeeleza.

NaCONGO imependekeza Jaji Mkuu wa Tanzania awe mwenyekiti wa kamati hiyo huku wa Jaji Mkuu Zanzibar akiwa makamu mwenyekiti na Jaji Kiongozi akiwa Katibu.

Wajumbe wake wawe ni naibu mwanasheria mkuu, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika na Zanzibar, Rais wa cha Majaji Wanawake Tanzania, Wawakilishi wawili kutoka kundi la Asasi za Kiraia waliofanya kazi katika eneo la utawala bora kwa zaidi ya miaka 10 na mmoja lazima awe mwanamke.

“Mwakilishi kutoka Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemav, na uwakilishi huo uzingatie jinsia,” ilieleza taarifa hiyo.

Pamoja na yote hayo, baraza hilo limependekeza nafasi ya ujumbe wa NEC na mkurugenzi ziwe zinaombwa kupitia kwa katibu wa kamati teule.

Baraza hilo limeshauri waombaji wawe na ubobevu usipungua miaka 15 katika taaluma ya sheria, ujaji au wakili mwandamizi viwe sehemu ya vigezo vya mtu kuwa mkurugenzi wa NEC.

“Asiwe mtu aliyewahi kujihusisha na siasa za vyama kwa muda wa miaka mitano kabla ya kuomba nafasi hiyo,” ilieleza taarifa hiyo.

Mapendekezo ya asasi hizo yanataka kushabihiana na yale yaliyokusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali na Kikosi Kazi cha Rais kisha kuwasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kufumuliwa kwa muundo na mfumo wa NEC ikiwemo namna ya kuwapata wajumbe na mwenyekiti wake na kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na NEC.


Sheria ya gharama za uchaguzi

Baraza hilo, limependekeza kuondolewa kwa maeneo yanayowatambua wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala na maofisa watendaji kata kuwa wasimamizi wa uchaguzi, badala yake jukumu hilo libaki kwa watumishi wa NEC.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa NaCONGO itaongeza uhuru na haki kwa tume.

Baraza hilo pia, limetaka sheria iweke masharti kwa vyama vya siasa kutenga fedha za kusaidia wanawake kugombea nafasi za ndani ya vyama, kadhalika viwafadhili kwenye kampeni za uchaguzi wa kitaifa.


Vyama vya siasa

Katika sheria hii, NaCONGO ilitaka ufafanuzi wa neno shiriki ili kuondoa utata wa vyama vya siasa nchini kushirikiana na vyama rafiki vya nje ya nchi.

“Neno “kushiriki” litolewe tafsiri kamili bila kuathiri ushirikiano wa vyama vya siasa vya Tanzania na vyama rafiki nje ya Tanzania kwenye programu mbalimbali za kujengeana uwezo,” ilisema.

Baraza hilo, lilitaka vyama vya siasa vipewe wajibu wa kutunga sera kali zinazozuia vitendo vya ukatili wa jinsia na kingono na katiba ziwawajibishe wanaobainika kuhusika navyo, ikiwemo kuwaondoa kwenye nafasi za uongozi.

Katika sheria hiyo, baraza hilo linataka maboresho yahusishe kuondolewa kwa ukomo wa ushirikiano au kuungana kwa vyama vya siasa, likisisitiza viruhusiwe kufanya hivyo kila vitakapoona inafaa.

Kuhusu utatuzi wa migogoro ya vyama, baraza lilitaka kuundwa kwa chombo kwa ajili ya shughuli hiyo na kiongozwe na mwenyekiti anayepaswa kuwa jaji mstaafu wa Mahakama Kuu na makamu mwenyekiti awe jaji mstaafu wa Mahakama Kuu kutoka Zanzibar na wote watateuliwa na Rais.

Pamoja nao, NaCHONGO inataka kuwepo wajumbe saba na kati yao, watatu wawe wanawake.

Lmetaka chombo hicho kishughulike na kusuluhisha mgogoro baina ya mwanachama na chama, chama na msajili wa vyama vya siasa, mgogoro kati ya chama cha siasa, muunganiko wa vyama na washirika wake na umoja wa vyama na wanachama wake.

Ingawa kilichopendekezwa ndiyo matakwa ya wadau wengi wa siasa, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakary alisema kilichofanyika si njia sahihi.

Alieleza ili kufanikisha maboresho ya sheria na maoni ya wadau, ilipaswa kwanza uandaliwe muswada kwa ajili ya kupelekwa bungeni.

“Huu utaratibu uliotumika si sahihi,” alisema mhadhiri huyo.