Watanzania 2,000 wanasoma Kichina

Muktasari:

Takribani wanafunzi 2000 wa Tanzania wanasoma lugha ya Kichina nchini, huku lugha hiyo ikitajwa kuambata na mafanikio kwa wale wanaojifunza.

Dar es Salaam. Takribani wanafunzi 2000 wa Tanzania wanasoma lugha ya Kichina nchini, huku lugha hiyo ikitajwa kuambata na mafanikio kwa wale wanaojifunza.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 10, 2022 jijini Dar es Salaam na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa waliofanya vizuri katika somo la kichina.

Amesema ufanisi katika kujifunza lugha ya kichina hauwezi kukamilika ndani ya siku moja, bali ni kutokana na uvumilivu wakati wa kujifunza.


"Kwa sasa, takribani wanafunzi 2000 hapa Tanzania wanasoma lugha ya Kichina. Kuna mifano mingi ya mafanikio kwenu katika kujifunza lugha ya kichina," amesema Balozi Mingjian.

Amesema mwishoni mwa mwaka 2021, nchi 16 za kiafrika zilikuwa zimeingiza somo la kichina katika mfumo wa taifa wa elimu na vyuo vikuu 30 vilikuwa vimekifanya Kichina kula somo ambalo wanafunzi wanaweza kujikita nalo.

"Walimu wazawa wa kichina na wanafunzi wanachangia katika urafiki wa China na Tanzania na kusaidia Watanzania wengi zaidi kupata uzoefu tofauti na kuujua ulimwengu," amesema Balozi huyo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Lyabwene Mutahabwa amemwomba Balozi Mingjian kukichukua Kiswahili kama lugha inayozungumzwa zaidi na kujifunza nchini kwao na kwingineko.


"Kiswahili ni moja kati ya lugha 10 kubwa duniani. Kwa hiyo ninawaomba rafiki zetu wa China, mkichukue kiswahili kama mnavyofanya kwenye lugha yenu. Mkifanye Kiswahili kizungumzwe sana huko China na duniani kote," amesema Dk Mutahabwa.

Amewapongeza wanafunzi wa Kitanzania kwa kujifunza na kuielewa lugha ya kichina. Amewahamasisha wanafunzi wengine wa shule za msingi na sekondari kujifunza lugha hiyo.

Washindi wa tuzo hizo ni wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Chuo Kukuu cha Dodoma (Udom), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) na Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro.

Washindi wengine ni pamoja na shule za sekondari za Benjamin Mkapa na Zanaki, zote kutoka mkoa wa Dar es Salaam.