Watatu wafariki ajalini, dereva atoroka

Muktasari:
- Watu watatu wamefariki dunia huku wengine watatu wakiwa ni majeruhi katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika mlima wa soda mikindani ambapo ilihusisha gari dogo, lori na pikipiki huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni mwando kasi.
Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limetoa taarifa ya ajali ya gari iliyoua watu watatu na kujeruhi wengine watatu katika eneo la Mikindani ajali iliyotokea majira ya usiku, huku chanzo kikitajwa kuwa ni mwendo wa kasi wa gari dogo.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP-Mtaki Kurwijila amesema kuwa ajali hiyo imesababisha vifo kwa abiria watatu waliokuwa katika gari ndogo.
Amewataja marehemu hao kuwa ni Mwanaidi Ahmed (51) mkazi wa Magomeni Mtwara, Mohamed Mfaume Mtumanuma (60) mkazi wa Ziwani na Niale Ally (32) mkazi wa magomeni wote wakazi wa Wilaya ya Mtwara.
Amesema kuwa mnamo Oktoba 10 majira ya saa tano usiku katika eneo la Mikindani Mlima wa Soda, Barabara ya Lindi- Mtwara ilitokea ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Alphad mali ya Abdallah Doa iliyokuwa ikiendesha na dereva aitwae Yahaya Juma Kasembe (35) mkazi wa Magomeni Mtwara akiwa na abiria saba.
Gari liligonjwa kwa nyuma aina ya Howo Truck mali ya Kampuni ya Saruji Dangote lililokuwa limeegeshwa pembeni kwa barabara baada ya kupata hitilafu na kisha kugonga pikipiki aina ya TVS ambayo haijafahamika namba zake iliyokuwa ikiwendeshwa na Diocles Leviana (25) mkazi wa Sabasaba.
Aidha ajali hio imesababisha majeruhi abiria watatu wa gari hilo na mpanda pikipiki mmoja mili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara na majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.
Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa gari ndogo na kushindwa kuchukua tahadhari ya kutosha barabarani ambapo aligonga gari jingine kwa nyuma kisha kumgonga mpanda pikipiki na kusababisha kifo. Dereva wa gari hilo dogo alitokweka kusikojulikana na juhudi zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa anakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Nitoe rai kwa watumiaji wa barabara hususani madereva wa vyombo vya moto wazingatie sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazogharimu maisha aya watu hatua kali za kisheria zinaendelea kuchukuliwa kwa wale wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani.
Meneja wa Kurugenzi ya Uuguzi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini, Dinnar Busunge amekiri hospitali hiyo kupokea miili ya watu watatu.
Amesema kuwa watu hao waliofariki ni wanawake wawili na mwanaume mmoja huku wakipokea majeruhi wanne ambao wanawake ni wawili na wanaume wawili waliopata ajali ya gari Mikindani majeruhi wawili wanaendelea vizuri na wataweza kiruhusiwa wakati wowote.