Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watoto 22, 000 waondolewa kwenye utumikishwaji

Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu, Suzan Mkangwa akizungumza katika kikao cha wadau cha kujadili utumikishwaji watoto mjini Tabora. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

Watoto zaidi ya 22,000 wenye miaka kati ya mitano hadi 17 wameondolewa kwenye kazi za utumikishwaji zikiwemo za mashamba ya tumbaku katika halmashauri tano za Chunya, Songwe, Kaliua, Urambo na Sikonge mkoani  Mbeya, Songwe na Tabora katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.

Tabora. Watoto zaidi ya 22,000 wenye miaka kati ya mitano hadi 17 wameondolewa kwenye kazi za utumikishwaji zikiwemo za mashamba ya tumbaku katika halmashauri tano za Chunya, Songwe, Kaliua, Urambo na Sikonge mkoani  Mbeya, Songwe na Tabora katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.

Meneja Mradi wa Prosper Reset unaojishughulisha na kuwaondoa watoto katika utumikishwaji, Fred Malaso ameeleza hayo Septemba 16, 2023 katika kikao cha kufuatilia mfumo wa masuala ya utumikishwaji watoto kilichohudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka vyama vya wafanyakazi, Chama cha Waajiri nchini, (ATE), wanunuzi wa tumbaku, maafisa ustawi na maendeleo ya Jamii wa halmashauri.

Malaso amesema watoto hao wamesaidiwa kwa kupelekwa shule pamoja na kupewa stadi za maisha, kufundishwa ufundi wa aina mbalimbali ukiwemo ujenzi, ushonaji, uashi ambazo zimewasaidia kuingiza kipato na kuachana na utumikishwaji.

“Hatukuwaacha pasipo kuwapa kitu cha ziada na ndio maana tumewapa ujuzi unaowasaidia huku wengine tukiwapeleka shuleni”amesema

Amesema wazazi na walezi wa watoto wanaosoma shule walipewa elimu ya ujasiriamali na kuanzisha vikundi 50 vyenye mitaji ya zaidi ya Sh180 milioni ambayo inakua na kuwasaidia.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Leonard Celestine amesema yawepo mazingira ya kazi yasiyohusisha mtoto ambayo yatakuwa na staha kwake.

“Lazima tupinge utumikishwaji watoto katika maeneo ya kazi na kutomhusisha mtoto  kabisa,”amesema

Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Suzan Mkangwa mbali na kupongeza ushirikiano wa wadau katika kupiga vita utumikishwaji watoto ,ametaka ushirikiano wa wadau wote kutokomeza ajira kwa watoto.

“Tunapongeza ushirikiano wa wadau wote na lengo letu liwe ni kutokomeza utumikishwaji watoto ambalo ndio lengo la Serikali,”amesema

Malengo ya kikao hicho ni kufuatilia mfumo wa masuala ya utumikishwaji watoto na kujadili namna bora zaidi ya kufuatilia masuala ya utumikishwaji watoto na upatikanaji wa taarifa kutoka ngazi za jamii.