Watoto watatu waliofariki kwa ajali ya moto waagwa

Muktasari:
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema ameongoza jopo la wananchi kuaga miili ya watoto watatu waliofariki juzi kwa ajali ya moto usiku katika shule ya msingi Buhangija katika manispaa ya Shinyanga baada ya bweni walimokuwa wamelala kuteketea kwa moto.
Shinyanga. Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema ameongoza jopo la wananchi kuaga miili ya watoto watatu waliofariki juzi kwa ajali ya moto usiku katika shule ya msingi Buhangija katika manispaa ya Shinyanga baada ya bweni walimokuwa wamelala kuteketea kwa moto.
Tukio la kuaga miili hiyo limefanyika leo 25,2022 katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga, ambapo mkuu wa mkoa Sophia Mjema amewapa pole wazazi na kuwaomba waendelee kuwa watulivu wakati zoezi la uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo ya moto ukiendelea.
Mjema amesema tukio hilo ni la kusikitisha sana, kwani watoto hao baadae wangesaidia wazazi wao, lakini kwa vile imetokea hivi hakuna namna ni kuendelea kumshukuru Mungu, pia serikali inaendelea kufanya uchunguzi wazazi waendelee kuwa na utulivu.
"Tunawatakia safari njema mfike salama kwa ajili ya kuwahifadhi watoto wetu serikali ipo pamoja nanyi,"amesema Mkuu wa mkoa Mjema.
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Charles Ngelela ambaye alizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa CCM mkoa amesema msiba huo umekiumiza sana chama cha mapinduzi CCM, ila wanaishukuru serikali kwa vile imekuwa bega kwa bega,pia amewaomba wazazi katika wakati huu mgumu wamtegemee Mungu atawaongoza, kila wilaya anapoenda kuzikwa mtoto atakuwepo kiongozi wa CCM wilaya.
Mwenyekiti wa chama cha shirikisho la watu wenye ulemavu Mkoa wa Shinyanga Richard Mpongo amesema tukio hilo limekuwa ni tukio la kushtua na la hudhuni, lakini ameiomba serikali iwe makini na shule za bweni iwe inaangalia miundombinu yake ya madarasa.
"Tunaishukuru serikali kwa ushirikiano wake ilioutoa, lakini pia shule hii ilijengwa mwaka 1965 imekuwa ni ya miaka mingi sana hivyo inaweza kuwa kisababisho, hivyo serikali iwe makini kwenye hizi shule za bweni, haya majengo ya zamani uchakavu pia unaweza ukawa unachangia ijapokuwa wanaendelea na uchunguzi wa tatizo hili,"amesema Mpongo.
Mwalimu anayefundisha shule hiyo Agnes Ngule amesema toka ianzishwe shule hiyo halijawahi kutokea tukio kubwa la namna hiyo, hivyo serikali iendelee na uchunguzi ili chanzo cha tukio hilo kipatikane.
Ibada ya kuiga miili hiyo imeongozwa na padri Adolfu Makandago kwa niaba ya Askofu Sangu wa jimbo la Shinyanga ambapo amewaomba wazazi waendelee kumshukuru Mungu kwani amewapenda zaidi .
Watoto hao watasafirshwa leo kupelekwa kwenye makazi yao ya milele,ambapo watapelekwa wilaya tofauti, wilaya Maswa, mkoa wa Simiyu mwingine Bariadi na mwingine Itilima.