Wawili wafariki dunia kwa kukanyagwa na tembo

Muktasari:

  • Watu wawili wamefariki dunia na wengine watatu wamejeruhiwa na tembo wilayani Newala wakiwa shambani hali ambayo imepelekea kata hiyo na kata ya jirani shughuli mbalimbali kusimama ikiwemo za shambani.

Mtwara. Watu wawili wamefariki dunia huku watatu wakijeruhiwa na tembo wakiwa shambani katika Kijiji cha Mnanje Halmashauri ya mji Newala mkoani Mtwara baada ya kuvamiwa na tembo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Mkuu wa Wilaya ya Newala, Alhaj Mwangi Rajabu Kundya amesema kuwa alipata taarifa ya wananchi wa Kata ya Nanguruwe kuvamiwa na tembo wakiwa katika shughuli zao ikiwemo kilimo.

Amesema kuwa tembo hao walijeruhi watu watano na wawili walifariki dunia na wengine wapo hospitali wakiendelea na matibabu.

“Siku ya jana tembo walionekana Kijji cha Rahaleo ambapo walivamia mwananchi na kumkanyaga ubavu na hali yake kuwa mbaya ambapo alipelekwa hospitalini na kuhamishiwa kupelekwa Ndanda kutokana na hali yake amefariki dunia," amesema.

Pia, eneo la Mnanje, Kata ya Nanguruwe ambaye naye amekanyagwa na amefariki dunia pia wananchi watatu aliwaona tembo akawafuata ili awaone kwa karibu kwa kuwa walikuwa walimparamia na sasa anaendelea na matibabu.

“Kuna mwingine aliona tembo akakimbia akapanda juu ya mkorosho ambapo tembo waliutikisa mpaka akadondoka na saa yuko hospitali anaendelea na matibabu ambapo mwingine alipowaona alipata hofu na akapoteza fahamu,” amesema.

“Tangu jana tumewasiliana na wanyama pori ambapo kundi moja limerejeshwa ambapo uelekeo wake ni kaskazini ya Msumbiji kundi hiko jingine ndiyo ambalo limejeruhi na kuua watu,” amesema Alhaj Kundya.

Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya  Halmashauri ya Newala Mji, Dk Kideyi Mzelela amesema kuwa tulipokea wagonjwa waliojeruhiwa na kwa kukanyagwa na tembo wakiwa na majeraha makubwa hivyo tumewapa rufaa na wengine wawili wamefariki dunia.

Diwani wa Kata ya Julia, Abdul Hakika Katani (Dudu) amesema kuwa katika kata yake tembo walipita na hawakujeruhi mtu ambapo walierekea katika Kata ya Nanguruwe ambapo waliua watu wawili na walijeruhi watu watatu.

“Jana wananchi walipomuona tembo kulizuka taharuki na siyo tembo mmoja wapo wengi hatujajua idadi yao kwa kweli amezua taharuki hadi muda huu wananchi wapo majumbani shughuli za maendeleo zimesimama kwa hofu ya uwepo wa wanyama hao,” amesema Katani.