Wazalishaji walia na gharama za ETS

Sunday January 09 2022
stempu pic

Mtaalamu wa Sera wa Shirikisho la wenye viwanda (CTI), Frank Dafa

By Ephrahim Bahemu

Dar es Salaam. Wakati Kamati ya Maboresho ya Sera za Kodi (Task Force on Tax Reform) inayohusika na matayarisho ya Bajeti ya Serikali ikikaribisha wadau kutoa maoni yao kuhusu bajeti ya mwaka ujao (2022/23), wenye viwanda nchini wanasema gharama za stempu za kielektroniki (ETS) ni changamoto.
Kamati hiyo itaanza kazi yake Februari 2022 na itakuwa ikipokea maoni ya wadau, kufanya uchambuzi na kufanikisha majadiliano ya masuala mbalimbali yanayohusu sera za kodi na usimamizi wake, mwisho wa kuwasilisha maoni hayo ni Februari 10.
Akigusia matamanioa yao katika mwaka mpya wa fedha ujao, Mtaalamu wa Sera wa Shirikisho la wenye viwanda (CTI), Frank Dafa aliliambia Mwananchi jana kuwa ETS inaongeza gharama za kufanya biashara hivyo jambo hilo linapaswa kutazamwa upya.
“Suala la gharama za ETS limekuwa ni mjadala wetu wa muda mrefu, tunafikiri sasa Serikali italiangalia upya. Hata kama sio kuondoa utaratibu huo, basi kupunguza gharama zake kwa sababu zilizopo sasa zinakwaza biashara,” alisema.
Dafa alisema pamoja na suala hilo la ETS, Serikali inapaswa kuweka ulinzi wa kikodi kwa viwanda vya ndani kwa kuongeza kodi kwa bidhaa zinazotoka nje, licha ya kuzalishwa hapa nchini lakini suala la marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Aidha, mamlaka ya mapato nchini (TRA) imekuwa ikisifia suala la kuanzishwa kwa ETS kwa maelezo kuwa limeongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti ukosefu lakini wafanyabisahara wamekuwa wakikosoa kwa kile kinachoelezwa kuwa kwao ni mzigo katika uendeshaji.
Miezi kadhaa iliyopita katika mkutano wa kujadili mustakabali wa sekta ya viwanda nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Leodger Tenga alisema suala la ETS limekuwa mzigo mkubwa kwa wenye viwanda kutokana na bei yake kuwa juu sana.
Alisema umefika wakati wa Serikali sasa kuacha kutumia kampuni inayotoa huduma hiyo na kutafuta kampuni ya ndani ambayo itatoa huduma kwa bei ndogo zaidi au kutafuta mbadala wa mfumo huo.
“Kwa bidhaa kama soda gharama ya ETS ni karibia nusu ya ushuru wa bidhaa hivyo, Kreti moja ya soda ushuru wa forodha ni Sh500 na gharama ya ETS ni Sh230. Bora fedha yenyewe ingekuwa inalipwa kwa shilingi au inabaki ndani lakini licha ya kuwa bidhaa zetu tunauza kwa Shilingi tunalipia gharama ya ETS kwa dola na mabilioni hayo yanaenda nje ya nchi wala hazinufaishi Taifa,” alisema.
“ETS hamna inachokifanya cha ajabu zaidi ya ‘real time counter’ ambayo TRA wanaweza kuona hamna cha ajabu pale, teknolojia ya ETS sio ‘Rocket Science’ nafikiri Serikali itafute mtoa huduma wa ndani ambaye atatoa huduma hiyo kwa gharama nafuu hata kama ni Serikali yenyewe kutengeneza mfumo huo” aliongeza.
Alisema kwa kuwa mkataba wao wa awali upo ukiongoni Serikali isiwaongeze mkataba mwingine na badala yake utafutwe mbadala wake.

Advertisement