Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazazi waijia juu Manispaa ya Moshi kuhusu wanafunzi kuhamishwa shule

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi JK Nyerere, Manispaa ya Moshi wakiwa ndani ya shule hiyo wakijadiliana jambo. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

 Wazazi wa wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi JK Nyerere, iliyopo Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wameijia juu halmashauri ya manispaa hiyo, kwa kutaka kuwahamisha wanafunzi zaidi ya 500

Moshi. Wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi JK Nyerere, iliyopo Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wameijia juu halmashauri hiyo, kwa kile kinachosemwa mpango wa kuwahamisha wanafunzi zaidi ya 500 bila ridhaa ya wazazi, baada ya shule hiyo kugeuzwa kuwa ya mchepuo wa Kiingereza.

Hatua hiyo, imekuja wakati shule zikitarajiwa kufunguliwa Jumatatu Januari 8, mwaka huu huku wazazi wa wanafunzi hao wakieleza kitendo cha kuwahamisha watoto wao bila makubaliano, ni kuwachonganisha wananchi na Serikali yao.

Akizungumzia malalamiko hayo, Mkurugenzi wa mansipaa hiyo, Mwajuma Nasombe amesema mabadiliko ya shule hiyo kuwa ya mchepuo wa Kiingereza yalikuwa ni ya muda mrefu na kwamba hawajakurupuka, huku akidai wazazi walishirikishwa.

"Ni kweli tuna shule inayoenda kuanza ya mchepuo wa Kiingereza kwa muhula huu wa mwaka 2024/25, tunakwenda kuanza Januari mwaka huu, sio kweli kwamba jambo hili limekuwa ni ghafla jambo hili ni mchakato wa muda mrefu na mchakato huu wazazi walishirikishwa kwenye vikao mbalimbali," amesema Nasombe.

"Kikao cha mwisho cha wazazi kilikaa 27/10/ 2023 na walitaarifiwa rasmi juu ya kusudio la manispaa kuanzisha shule yake binafsi yenye mchepuo wa Kiingereza, hivyo tumeruhusu kila mzazi afike shuleni aseme ni shule ipi ipo karibu na itakuwa rahisi kwa mtoto wake kumhamishia, kwa hiyo mzazi akifika shule na kututajia tutamfanyia mpango wa kumhamisha shule hiyo.”

Hata hivyo, wazazi hao wamesema kikao cha mwisho cha bodi ya shule walielezwa juu ya kubadilishwa kwa shule hiyo kuwa ya mchepuo wa Kiingereza huku wakihakikishiwa kuwa itaanza na wanafunzi wapya wa darasa la kwanza.
Jana Alhamisi Januari 4, wazazi hao walipewa barua inayowapa maelezo ya kuwaondoa watoto wao shuleni hapo, huku wakitakiwa kuchagua shule wanazotaka wahamie.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wazazi hao, wamedai kuwa, awali walikubaliana wanafunzi wa darasa la pili hadi la saba wataendelea na masomo kama kawaida huku wakipokewa wa mchepuo mpya kwa madarasa ya awali na la kwanza.

Elibariki Akyoo, mmoja wa wazazi na mjumbe wa kamati wa shule hiyo, amesema: "Tulikaa kikao baada ya kuambiwa hii shule itakuwa ni ya mchepuo wa Kiingereza, tukakubaliana wanafunzi wa darasa la pili hadi la saba waendelee, cha kusikitisha tumeambiwa tuhamishe watoto tuwapeleke shule nyingine."

"Leo hii darasa la nne ni la mitihani, tunawapeleka wapi hawa watoto, lakini cha kushangaza, wazazi tunaambiwa tujaze fomu tuhamishe watoto wetu, wanataka tuwapeleke wapi na kwa misingi ipi?

“Kwa nini wanasubiri shule zinafunguliwa ndiyo wanatuamuru tuhamishie watoto shule ambazo wamepanga wao, hiyo sio sawa,” amelalamika mzazi huyo.

Kwa upande wa Godfrey Shao, mjumbe wa kamati ya shule, amesema: “wazazi hawana taarifa za kuwaondoa wanafunzi shuleni hapo, baadhi ya wazazi wanapigiwa simu kwenda shuleni na wanapofika wanaelezwa kuwa wanatakiwa wajaze fomu za watoto wao kujiunga na shule nyingine.”

"Tuliambiwa tutaonana na Mkurugenzi wa Manispaa na Meya, mpaka sasa hatujawaona hapa na shule Jumatatu zinafunguliwa, hatukatai maendeleo tunachotaka ni utaratibu mzuri uwekwe kwa maridhiano na wazazi nao wakubali," amesema.

Happy Ngowi, ambaye ni mmoja wa wazazi, amesema alipigiwa simu ikimtaka kufika shuleni hapo, na alipofika alitakiwa kujaza fomu kwa kuchagua shule anayotaka ampeleke mtoto.

Amesema shule hizo zilikuwa zimeorodheshwa kwenye ubao wa matangazo shuleni hapo, jambo ambalo amesema limemfedhehesha.

"Serikali watafute namna nyingine nzuri, inakuwaje leo ghafla wanatuambia vitu ambavyo hatuvielewi, na Jumatatu ni shule, hata kama tunahamisha watoto tuandaliwe utaratibu mzuri wakuhamisha watoto wetu, tusikurupuke kuwahamishia shule nyingine ambazo hatujui mazingira yakoje," amesema.