Wazazi watajwa kuwa chanzo ukatili kwa watoto

Baadhi ya wakazi wa kata ya Mgusu wilayani Geita wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsi dhidi ya Wanawake na watoto

Muktasari:

Watoto kutumika kwenye shughuli za kiuchumi ikiwemo kuuza karanga na ndizi kwenye maeneo ya mikusanyiko, vimetajwa kuwa sababu za watoto kufanyiwa ukatili wa kingono ikiwemo kubakwa na kulawitiwa.

Geita. Wakati Tanzania ikiadhimisha siku 16 za kupinga ukatili kwa jamii, wazazi wametajwa kuwa vinara wa ukatili wa kiuchumi kwa watoto kutokana na wao kuwatumikisha kwenye shughuli za kujipatia kipato na kuwanyima fursa ya kupata elimu.

Akizungumza leo Novemba 26, 2022 katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili yaliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la huduma za kujitolea (VSO) mmoani hapa, Mkaguzi wa Polisi kata ya Mgusu,  Alfred Nkoma amesema tabia hizo zimechochea ukatili wa kingono ikiwemo kubakwa na kulawitiwa.

“Wanawake mnawakatili watoto bila kujua, unamkuta mama kamtuma mtoto kwenda kuuza mkaa wengine ndizi na vitumbua muda ambao wenzake wako darasani wengine jioni hadi usiku wanatembeza ndizi au karanga baa huu ni ukatili.

 “Geita shughuli kubwa ni madini, hasa wakati huu wa mvua watoto wanatumwa porini kuchukua kuni kwa ajili ya kuchoma udongo wa dhahabu, huko wanafanyiwa ukatili wanabakwa na kulawitiwa,” amesema Nkoma.

Kwa upande wake Mkuu wa ushirikishwaji jamii kutoka Jeshi la Polisi wilaya ya Geita, Grace Kaijage amesema changamoto iliyopo kwenye jamii kwa sasa ni wanawake kuwa watafutaji wa pesa zaidi na kusahau wajibu wao wa malezi kwenye familia.

“Kutafuta pesa ni jambo zuri, lakini simamieni familia kwa kuwa vitendo vya ukatili vinafanyika nyumbani wale mnaowaaamini ndio hao hao wanawakatili watoto ni wajibu wako kusimama kwa ajili ya hatma ya watoto wako,” amesema Kaijage.

Kaijage amesema changamoto kubwa iliyopo maeneo ya Geita ni wakazi wake kuona ukatili kama jambo la kawaida na hata linapofichuliwa hawapo tayari kutoa ushahidi hivyo kusababisha mashtaka kufutwa mahakamani.

Naye Ofisa Jumuishi na Usawa kutoka shirika lisilo la kiserikali la VSO, Hellen Mahindi ameitaka jamii kuondoa usiri na kujenga jamii inayojitambua na kufikiri kwa upya katika mstakabali wa usawa wenye matumaini.

Hakimu wa mahakama ya Mwanzo Nyankumbu Devotha Kasebele, amesema wivu wa mapenzi ndio unaosababisha ukatili kwa wanawake na kuwataka kutofumbia macho vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa na wenzi wao.

Baadhi ya wananchi akiwemo Asia Mohamed mkazi wa Geita amesema ili kukabiliana na vitendo vya ukatili, viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kubeba ajenda ya kupinga ukatili wakati wa ibada.