Waziri awataka wataalamu wa Tehama kusaidia Zanzibar kiuchumi
Muktasari:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk Saada Mkuya, amesema Serikali inafanya mageuzi ya kiutendaji kitaasisi na kimifumo hivyo ni vyema watalamu waisaidie kufikia malengo yake.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imezisisitiza taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinatumia mifumo ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama) iliyowekwa ili kwenda na mabadiliko ya dunia na kukuza uchumi kupitia biashara mtandao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk Saada Mkuya ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 29, 2022 wakati akifungua mkutano wa siku moja wa usimamizi na uendeshaji wa mifumo ya Tehama katika utoaji wa huduma kwa umma na ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Amesema Serikali inafanya mageuzi makubwa ya kiutendaji kitaasisi na hata kimifumo hivyo ni vyema watalamu wa Tehama kutambua umuhimu mkubwa wa kuisaidia Serikali kufikia malengo yake.
“Uchumi wa kidijitali hivi sasa ni uchumi ambao Zanzibar haiwezi kuepukana nao kwani dunia ipo huko hivyo ni lazima kujikita katika kuwezesha katika uchumi wa kidijitali na dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050,” amesema
Waziri Saada, amesema kulingana na mazingira ya sasa wataalamu wa Tehama wanahitajika kuwa mstari wa mbele zaidi katika kuanzisha mifumo ambayo itakuwa na tija kwa nchi katika taasisi zao.
“Ninyi mna umuhimu mkubwa kwani mnahitajika kuliko vile ambavyo nyinyi mnahisi, umuhimu wenu sasa ni lazima taasisi na uongozi kwenda katika mifumo ya kidijitali na watu wa IT kwenda mbele zaidi kuweka mifumo katika taasisi zenu,” amesema
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala Serikali Mtandao e- Government, Said Seif Said, amesema Serikali inawekeza kwa kasi kubwa katika uwekaji wa mifumo ya Tehama.
Amesema ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali, Wakala wa serikali mtandano inafahamu kuwa jitihada kubwa zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha lengo la uletwaji wa mifumo hiyo linafanikiwa.
Mkutano huo una lenga kuhamasisha utumiaji wa mfumo wa ununuzi kwa njia ya mtandao ambapo jitihada zinatakiwa kuchukuliwa katika usimamizi na uendeshaji wa mfumo huo kwa watendaji wa Serikali na watoa huduma.