Waziri, mfanyabiashara wafikishana kortini

Muktasari:
NUKUU: “Maghembe aliibuka na kielelezo cha barua yenye nembo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Wizara ya Maji ya kumpa madaraka Twaibu Maghembe Kusimamia shamba.” Mwita Marwa
Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe anahusishwa katika kesi ya uvamizi wa shamba lililopo eneo la Madale jijini Dar es Salaam, iliyofunguliwa na mfanyabiashara Mwita Marwa Kisiboye katika Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kinondoni.
Kwa mujibu wa kesi hiyo namba 332 ya 2013 itakayoendelea kusikilizwa Septemba 23, 2014 na Mwenyekiti wa Baraza hilo, E. D. Mtunga, Mwita anadai kuwa ndugu wa waziri huyo, Twaibu Maghembe amevamia eneo lake la ekari tano lililopo eneo la Madale Kunduchi.
Mwita ambaye anatetewa na Wakili Benjamin Mwakagamba kutoka Kampuni ya Uwakili ya BM, anadai kuwa yeye ni mmiliki halali wa eneo hilo na kwamba alilinunua tangu mwaka 2002 kutoka kwa Zuberi Ally Tendele kwa gharama ya Sh8 milioni na kwamba halikuwahi kuwa na mgogoro wowote.
Alidai kuwa Juni 2013 akiwa safarini alijulishwa na mtu ambaye alimuuzia eneo hilo, Tendele kuwa kuna mtu amevamia eneo lake na kuanza ujenzi, akamwambia apeleke taarifa Serikali ya mtaa na akazipeleka kwa Mwenyekiti Rashid Jumanne, ambaye alimwita akakataa kwenda na hatimaye akafungua kesi hiyo.
Aliendelea kudai kuwa baada ya kufungua kesi hiyo, Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kinondoni , Novemba 8, 2013 lilitolea amri shamba hilo lisiendelezwe na mtu yeyote hadi shauri la msingi litakaposikilizwa, lakini Twaibu Magembe alikaidi na na kuendelea kuliendeleza eneo hilo.
Mwita kupitia wakili wake, Mwakagamba alidai kuwa wakati hayo yakiendelea Twaibu Maghembe aliibuka na kielelezo cha barua yenye nembo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Wizara ya Maji, yenye kumbukumbu namba JAM/ PERS/DSM/01 ya Aprili 5/2014 ya kumpa madaraka Twaibu Maghembe ya Kusimamia shamba lenye ukubwa wa ekari 16, likiwemo eneo la ekari 5 ambalo Mwita anadai kuwa ni mali yake halali.
Kwa mujibu wa barua hiyo ya Profesa Maghembe anamwarifu yeyote anayehusika kuwa amempa madaraka kamili ya usimamizi wa shamba lake hilo na kuomba apewe msaada wote atakaohitaji ili aweze kulitumia. Alidai kuwa licha ya kuwasilisha barua hiyo, Twaibu ambaye anatetewa na Kampuni ya Uwakili ya Msemwa aliwasilisha hati ya utetezi katika baraza hilo la ardhi akionyesha yeye ni mmiliki wa eneo hilo na siyo Profesa Jumanne Maghembe, ambaye pia amempa nguvu ya kisheria kulisimamia iliyosajiliwa.
Mwita amedai kuwa na hati za ununuzi wa eneo hilo,pia amepanda mazao ya kudumu na halikuwahi kuwa na mgogoro hadi Juni 2013.