Waziri Mkenda asema ufaulu somo la hisabati ni janga linalotakiwa kutafutiwa ufumbuzi

Muktasari:
- Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ufaulu wa somo la hisabati ni janga ambalo halitakiwi kufumbiwa macho badala yake kutafutiwa ufumbuzi.
Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ufaulu wa somo la hisabati ni janga ambalo halitakiwi kufumbiwa macho badala yake kutafutiwa ufumbuzi.
Hivyo ameagiza Idara ya Hisabati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kufanya utafiti ili kubaini chanzo cha wanafunzi wengi kufeli somo hilo kwenye Mtihani wa Kidato cha nne.
Waziri Mkenda aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa walimu ambao wanafunzi wao wamefanya vizuri katika somo la Hisabati wilayani Ubungo zilizoandaliwa na Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo.
Amesema bado kuna changamoto katika somo la hisabati ambapo inatakiwa kuchukuwa hatua za haraka ili kuweza kuitatua changamoto hiyo.
Profesa Mkenda amesema kwa mwaka 2021 hali ya ufaulu kwa somo la hisabati kidato cha IV ni mbaya hali iliyolazimu kufanyika kwa utafiti ili kujua sababu za wanafunzi kutokufanya vizuri.
“Hesabu ni janga ambalo halitakiwi kulifumbia macho, inatakaiwa kutafakari na kuchukua hatua. Wenzetu duniani nchi zilizoendana, bado wanawashindanisha kwa uwezo wa wanafunzi wao kufaulu hasa katika somo la hisabati…kwahiyo sisi hii haturidhiki nayo lazima tuchukue hatua za haraka,"
Kwa upande wake Mbunge wa Ubungo, Profesa Mkumbo amesema ameanzisha programu ya KiuHisabati ili kuchochea ari ya Walimu kufundisha somo hilo na wanafunzi kujifunza wakijua kuwa ipo motisha kwao pindi wanapofanya vizuri
Profesa Kitila amesema katika tuzo hizo walimu ambao wanafunzi wao wamefanya vizuri katika somo la Hisabati kidato cha IV mwaka 2021 wamepatiwa Sh100,000 kwa kila mwanafunzi aliyepata Alama A.
Mbali na Motisha hiyo kwa walimu, Profesa Mkumbo amesema atawalipia ada ya masomo ya Kidato cha V na VI wanafunzi wote waliopata alama A kwa somo la Hisabati huku waliopata alama B wakilipiwa nusu ya ada kwa kidato cha V na VI.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kheri James amesema ukizungumzia uimara wa masomo yote msingi wake ni Hisabati na pale mwanafunzi anapofanya vizuri kwenye Hisabati na masomo mengine anafanya vizuri pia.
Naye Katibu wa Chama cha walimu wa Hisabati ambaye pia ni mhadhiri wa UDSM Idara ya Hisabati, Dk Said Sima amesema uzoefu unaonesha changamoto kubwa iliyopo katika somo la hisabati inatokana na uchache wa walimu wanaofundisha somo hilo.
“Pia maneno ya watu kukatishana tamaa kwamba Hisabati ni somo gumu, hii dhana inatakiwa iondolewe, watu walichukulie somo hili kama yalivyo masomo mengine,” alisema Dk Sima.