Waziri Mkuu kuongoza mkutano tathmini sekta ya mkonge Tanga

Waziri mkuu Kassim Majaliwa.

Tanga. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Tathmini ya Maendeleo ya Zao la Mkonge 2020–2023 Machi 6, mwaka huu jijini Tanga.

Akizungumzia ujio huo wa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona amesema mkutano huo ni muhimu  kwani pamoja na mambo mengine utatoa tathmini ya mwelekeo wa zao la Mkonge nchini kwani utajadili utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu aliyotoa mwaka 2020.

“Kama mnavyokumbuka Machi mwaka 2020 Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa Tanga kupokea taarifa ya timu ambayo alikuwa ameiunda ya kufuatilia mali za iliyokuwa Mamlaka ya Mkonge Tanzania, ni katika kipindi hicho ndiyo serikali ilikuwa imechukua hatua za makusudi katika zao la Mkonge.

“Waziri Mkuu baada ya kupokea taarifa, alifanya mabadiliko makubwa na kutoa maelekezo mengi ya kufanyia kazi ambayo yalihusisha mabadiliko ya uongozi na kutoa maelekezo mbalimbali ya kufanyia kazi kuleta mapinduzi kwenye tasnia ya Mkonge,” amesema Mkurugenzi Kambona.

Mkurugenzi Kambona amesema ni mwaka wa tatu tangu Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo na sasa anakuja kwa ajili ya kufanya tathmini ya maendeleo ya Mkonge kuona wapi ilikuwa na wapi ipo na ikizingatiwa kwamba liko lengo kubwa la serikali la kuhakikisha wanaongeza uzalishaji kutoka tani 36,000 kwa kipindi kile cha 2020 hadi kufikia tani 120,000 mwaka 2025/26.

“Kwa hiyo ni mkutano muhimu na tunawakaribisha wadau wote kuja kwa ajili ya kujadili pamoja na kushauri masuala mbalimbali kuona wapi tumepatia, wapi tumekosea na tufanye nini ili kuyafikia yale malengo ya serikali tuliyowekewa.

“Tufike tujadiliane ili Waziri Mkuu naye atupe maelekezo mengine pale ambapo tumepatia, aone na atuelekeze nini cha kufanya ya kule tunakotaka kufika,” amesema.