Waziri Silaa asimamisha ujenzi wa kituo cha mafuta Moshi

Waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya Majazi, Jerry Silaa (kushoto) akikagua ramani wakati alipokagua ujenzi wa kituo cha mafuta kata ya Mawrnzi Manispaa ya Moshi. Picha na Florah Temba

Moshi. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa ameagiza uongozi wa Manispaa ya Moshi, kusimamisha ujenzi wa kituo cha mafuta katika eneo la Shabaha, Kata ya Mawenzi, mpaka hapo Wizara itakapotoa maamuzi.

Silaa ametoa agizo hilo leo Oktoba 5, 2023, wakati alipofika akikagua eneo ambapo kituo hicho kinajengwa, huku akisema liko chini ya mita 200 kutoka kilipo kituo kingine cha mafuta cha Puma.

Waziri Silaa baada ya kupokea taarifa na kupitia ramani ya eneo hilo, ameagiza kusimamishwa kwa ujenzi huo, na kueleza kuwa ni hatari kutokana na umbali kilipo kituo hicho na kituo kingine.

"Uongozi wa Manispaa, simamisheni ujenzi huu, nitatoa maelekezo baadae, kwani mlitengeneza sheria ambazo zitakuja kuleta matatizo hapo baadae, kabla sijatoka Moshi nione hiyo stop oder," amesema Silaa.

Baada ya kauli hiyo, mmiliki wa eneo hilo, Ibrahim Shayo, aliomba kufahamu sababu za ujenzi huo kusimamishwa.

"Samahani Waziri, mimi kosa langu ni nini mpaka kufikia hatua ya kusimamisha ujenzi, mimi kama mfanyabiashara mnyonge ningetaka kujua," amesema Shayo huku waziri akimkatisha na kumtaka asimfanye aonekane mbaya.

Waziri Silaa yupo katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Kilimanjaro, ambapo pamoja na kukagua eneo hilo la ujenzi wa kituo cha mafuta, atakagua maeneo yanayodaiwa kuwa na migogoro ikiwemo uwanja wa ndege Moshi na kuzungumza na watumishi.