Waziri Ummy: Inasikitisha madaktari kuombana rushwa

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

  • Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema rushwa imekithiri na kuota mizizi katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) kiasi cha madaktari kuombana rushwa wenyewe kwa wenyewe.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema rushwa imekithiri na kuota mizizi katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) kiasi cha madaktari kuombana rushwa wenyewe kwa wenyewe.

Ummy aliyasema hayo juzi, alipozindua bodi mpya ya wadhamini wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akiwa na viongozi waandamizi wa taasisi zilizo chini ya wizaya hiyo.

“Kati ya hospitali mbili ambazo nalala usingizi ni JKCI na Benjamin Mkapa ya Dodoma. Ni kati ya hospitali za Serikali zinazofanya vizuri. JKCI huwezi kusikia malalamiko ya hovyohovyo kutoka kwa wagonjwa, ikiwamo uombaji rushwa. Nimekaa Wizara ya Afya miaka mitano na sasa nina miezi sita sijawahi kusikia mgonjwa ameambiwa sijui leta hela au anazungushwazungushwa,” alisema na kuongeza:

“Nawaagiza waganga wafawidhi nendeni mkajifunze JKCI, (Profesa Mohamed) Janabi anafanya kitu gani. Benjamin Mkapa nako hakuna malalamiko ya hovyohovyo ila MOI panasikitisha…yaani daktari anamuomba rushwa daktari mwenzake, imefikia hatua mpaka wanaanikana kwenye magrupu kwa mtaalamu mwenzie kumuomba rushwa halafu huyo mtu analipwa mshahara, wanachukua asilimia 70 ya fedha za NHIF lakini nisiharibu mkutano nitaenda kusema nikifike kule.”

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy aliiagiza bodi hiyo kupunguza gharama za matibabu bila kuathiri ubora wa huduma na uongozi wa JKCI kuhakikisha wanahamishia huduma zao katika kituo cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kampasi ya Mloganzila ambayo ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa kwanza Zanzibar, Othman Masoud Othman.

“Hapa pameshakuwa pafinyu, angalieni namna ya kutoka muende Mloganzila ili mtoe huduma katika eneo kubwa na wagonjwa wapate nafasi ya kufanya mazoezi,” alisema Waziri Ummy.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Janabi alisema hospitali hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015 ina vitanda 150 vya kulaza wagonjwa, 37 vya wagonjwa mahututi na vinne vya wagonjwa mashuhuri.

“Tangu kuanzishwa kwa taasisi hii wagonjwa 10,819 wamefanyiwa upasuaji. Mpaka sasa tumehudumia jumla ya wagonjwa 600,006 hivyo taasisi kuokoa Sh51 bilioni ambazo zingetumika iwapo wagonjwa hao wangekwenda nje ya nchi,” alisema Profesa Janabi.