Wengi wajitokeza kuaga mwili wa Ole Mushi
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Thadei Mushi aliyekuwa kada wa CCM wakiingiza katika Kanisa Katoliki lililopo Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya ibada ya kuaga kabla ya kusafirishwa kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mazishi. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Dada wake aishukuru Serikali, ndugu, jamaa na marafiki kwa misaada yao.
Dar es Salaam. Mwili wa mchambuzi na mchangiaji mada kwenye mijadala mitandaoni, Thadei Ole Mushi umeagwa jijini Dar es Salaam, huku familia ikiishukuru Serikali na wadau kwa namna walivyojitoa kumsaidia ndugu yao.
Mwili wa Ole Mushi aliyefariki dunia Jumapili Februari 4, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa amalazwa kwa matatizo ya moyo, umeagwa leo Jumanne, Februari 6, 2024 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Maziko yatafanyika Jumatano, Februari 7, 2024 nyumbani kwao Moshi.
Christina Mushi, dada wa Ole Mushi ameishukuru Serikali kwa namna ilivyowasaidia kwenye matibabu.
"Thadei amesaidiwa sana, yamesemwa mengi ila sisi familia ndio tunajua na Mungu anajua," amesema.
Christina amewashukuru ndugu jamaa na marafiki wa Thadei kwa namna walivyojitoa kumsaidia wakati wote akiugua.
"Tunashukuru kwa maisha yake, lakini pia tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumsaidia kwa kipindi chote ambacho ndugu yetu alikuwa anaumwa. Pia Victor (Tesha), ambaye ni rafiki wa Thadei amemsaidia, ameshiriki kwenye mambo mengi tunaomba asikate tamaa," amesema.
Amesema Ole Mushi alikuwa mtoto wa mwisho kwenye familia yao ya watoto watano.
Waombolezaji wakiwa katika ibada ya kuaga mwili wa Thadeo Mushi katika Kanisa Katoliki lililopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mazishi. Picha na Said Khamis
Akitoa salamu kwa niaba ya Serikali, mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe amesema Ole Mushi alikuwa mshauri kwenye masuala ya elimu na yake binafsi ya kisiasa.
"Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya Ole Mushi, alikuwa sehemu ya maisha yetu, alikuwa mpambanaji wa jimbo la Hai, ofisa elimu taaluma katika wilaya hiyo,” amesema Mafuwe.
Amewataka marafiki zake kuendelea kuenzi yale yote aliyokuwa anayaishi na kuamini kuwa yatatokea kwenye familia.
Katibu wa Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga amesema chama hicho kitaendele kumuenzi kwa mafundisho na machapisho yake aliyokuwa akitumia kutoa elimu kwa jamii. Ole Mushi alikuwa kada wa chama hicho.
Akihubiri wakati wa misa, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria Salama ya Wagonjwa -Muhimbili, Patrick Bwakila amemshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Ole Mushi kupitia makala mbalimbali alizokuwa akiandika.
Amesema kuna kila sababu ya mtu kuheshimu maisha ya mwingine kwa vile mtu atakuwa mpumbavu kama hatatumia alichopewa kwa ajili ya wengine.
"Twende tukatimize wajibu wetu, utakuwa mpumbavu kama hutaheshimu wengine au hutafanya kile ulichopewa kwa ajili ya wengine," amesema.
Amebainisha kila mmoja atimize wajibu wake, kama ni mwalimu akafundishe, mwandishi akafanye kazi yake na wengine wakafanye kulingana na taaluma zao bila kupotosha.
"Waandishi mkapeleke taarifa za kutia watu moyo na si za kunyong’onyesha wala kuhuzunisha, leo hii Thadei hayupo tukaandike habari njema watu wajue alikuwa ni nani katika jamii na kuonyesha mchango wake katika Taifa," amesema na kuongeza:
"Tufuate desturi zilizo njema, kuchunguza afya zetu mara kwa mara, kutunza miili yetu kwa kuwa ni hekalu la Roho Mtakatifu, kuleni kwa kiasi na kunywa kwa kiasi tujitunze na kutunza ndugu zetu."
Wasifu wa Ole Mushi
Colman Mushi, akisoma wasifu wa Ole Mushi amesema alizaliwa Kijiji cha Shinga, Kata ya Uru Kusini, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema Ole Mushi ambaye kitaaluma ni mwalimu, aliwahi kuhuduma katika shule mbalimbali mkoani Kilimanjaro.
Mwaka 2006-2014 alikuwa mwalimu mkuu msaidizi wa Shule ya Msingi Masoka, mwaka 2015 -2019 alikuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Kirimajuu.
Amesema mwaka 2020 alikuwa mratibu elimu kata ya Marangu Magharibi na kuanzia Oktoba 2020 mpaka alipofikwa na umauti alikuwa Ofisa Elimu taaluma sekondari katika Wilaya ya Hai.