Wenyeviti wa mikoa wa Chadema wamtembelea Mbowe gerezani akitimiza siku 90

Monday October 18 2021
mBOWE PC
By Peter Elias

Dar es Salaam. Wenyeviti wa mikoa wa Chadema, wamemtembelea mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe katika gereza la Ukonga ili kumjulia hali na kumtia moyo katika kesi inayomkabili.

Mbowe anayekabiliwa na kesi ya ugaidi na leo ametimiza siku 90, tangu alipokamatwa mkoani Mwanza ambako alikuwa akiongoza kikao cha kuhamasisha kupatikana kwa katiba mpya.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Oktoba 18 mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa msafara huo, William Mungai ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Iringa, amesema wamekuta Mbowe ana afya njema na yuko imara katika mapambano.

Soma hapa: Utata waibuka alipo mtuhumiwa kesi ya kina Mbowe

"Tumemwona mwenyekiti yuko imara na ametuhakikishia kwamba afya yake ni njema katika mazingira aliyopo. Yupo anajisomea vitabu, tunaamini akitoka atakuwa bora zaidi," amesema Mungai wakati akizungumza na vyombo vya habari.

Amewataka wananchi waendelee kufuatilia kesi ya kiongozi huyo ambayo itaendelea Oktoba 20 huku akisisitiza kwamba chama kitaendelea kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kwa sababu ndiyo mahitaji ya sasa.

Advertisement

Soma hapa: Ushahidi wa RPC Kinondoni kesi ya kina Mbowe huu hapa

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Njombe, Rose Mayemba amesema licha ya Mbowe kushikiliwa mahabusu, bado chama hicho kiko imara kwa sababu alitengeneza viongozi wengine wenye uwezo wa kupambana kwa niaba ya wananchi.

"Mbowe kuwa gerezani, haijarudisha nyuma harakati za chama, tuko imara, tutaendelea kuwa imara na hii inatukumbusha Watanzania kwamba kama Mbowe, mwenyekiti wa chama taifa anatiwa gerezani, wewe je? Uko katika hali gani?" anahoji mwenyekiti huyo.

Advertisement