Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yas yazindua huduma ya uchunguzi wa macho bila malipo Sabasaba

Muktasari:

  • Zaidi ya wananchi 25,000 wamefaidika na kampeni ya “Afya ya macho kwa wote” tangu kuanzishwa kwake

Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Yas leo imezindua rasmi huduma ya uchunguzi wa macho bila malipo kwa wananchi wanaotembelea banda lake lililopo katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Huduma hiyo inayotolewa kwa kushirikiana na KSI Charitable Eye Centre, inajumuisha, uchunguzi wa macho, upimaji na ugawaji wa miwani, na matibabu ya matatizo kama mzio na vumbi.

Pia kupitia uchunguzi huo watakaobainika na changamoto kubwa wanapatiwa rufaa hususan wanaohitaji kufanyiwa upasuaji ukiwemo wa mtoto wa jicho.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Yas, Rukia Mtingwa, amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo ya kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo ya jamii ya Kitanzania.

“Kuona ni haki ya msingi ya kila binadamu. Kwa bahati mbaya, Watanzania wengi hususan wa kipato cha chini na wanaoishi vijijini au kwenye maeneo yenye huduma hafifu za afya, wanakosa huduma za macho. Yas tumeamua kuja kivingine si tu kama mtoa huduma za mawasiliano, bali kama mshirika wa maisha ya kila siku ya Mtanzania,” amesema Mtingwa.

Huduma hiyo ni sehemu ya kampeni ya “Afya ya Macho kwa Wote”, iliyoanzishwa na Yas mwaka jana. Tangu kuanzishwa kwake, kampeni hii imewafikia zaidi ya wananchi 25,000 katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Mtwara, Pwani, Unguja na Pemba. Yas inatarajia kuwafikia maelfu zaidi kupitia maonesho ya mwaka huu.

“Kama kampuni ya kidijitali, tunaamini hakuna maana ya teknolojia kama mtu hawezi kuona. Teknolojia bila afya ni sawa na mwanga bila macho. Ndio maana tumechukua hatua za makusudi kusaidia jamii kwa vitendo,” amesisitiza.

Huduma ya macho itatolewa kila siku katika banda la Yas hadi kufikia mwisho wa maonesho ya Sabasaba, ikiwa wazi kwa wananchi wote bila gharama yoyote.

Mtingwa pia alitoa shukrani kwa KSI Charitable Eye Centre kwa utaalamu wao wa hali ya juu na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa kuruhusu huduma hii kufanyika kwa mafanikio makubwa.

“Uoni bora si afya tu – ni fursa ya kuona familia yako, kujifunza, kufanya kazi, kuendesha biashara, na kutumia huduma za kidijitali kama Yas na Mixx. Tunawakaribisha wote kwenye banda letu,” amehitimisha.

Kwa upande wake mshiriki katika maonyesho hayo, Hajira Salum ameitaka Yas kuendeleza utamaduni huo kwa kile alichodai unasaidia kufikisha huduma ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa kwa wananchi hasa kwenye kipato cha chini

“Kuna watu hawawezi kumudu gharama za matibabu ila kupitia huduma na ofa kama hizi wanapatiwa huduma hizo. Tunawashukuru na kuwapongeza Yas,” amesema Hajira.

Naye, Munuo Sillo ameyashauri mashirika na taasisi nyingine kujitolea kusaidia upatikanaji wa huduma.