Zena Said afichua siri safari yake ya uongozi

Zena Said afichua siri safari yake ya uongozi

Muktasari:

  • Anasema usifanye kazi ili uonwe na wakubwa kisha uteuliwe, acha kazi yako ikutangaze mbele ya nyuso za watu

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zanzibar, Zena Said ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dk Hussein Mwinyi.

Mwanamke huyo, ambaye kwa nafasi yake ni mtendaji mkuu wa Serikali hiyo, anafichua siri kwamba kuipata nafasi hiyo si kwa sababu nyingine yoyote ile iwayo, bali ni kudra za Mwenyezi Mungu, utii, kujituma, kuthamini kazi, moyo wa kujifunza, nidhamu na utendaji kazi. Mapema wiki iliyopita, Mwananchi lilifanya mazungumzo maalumu na mwana dada huyu katika Ofisi za Ikulu mjini Unguja. Anasema kila nafasi anayoipata anajitahidi kufanya kwa bidii ili aweze kuendana na kasi inayokuwapo katika sehemu husika.

Zena Said afichua siri safari yake ya uongozi

Mwananchi lilitaka kufahamu anazungumziaje suala la mwanamke na uongozi. Zena anasema huo ni utumishi kama zilivyo kazi nyingine, hivyo mwanamke akipata nafasi ya kuongoza mahala popote, hana budi kudhihirisha kwamba hajateuliwa au kuchaguliwa kwa kubahatisha. _“Kikubwa ni kujitahidi kufanya kazi ili ukipewa nafasi isionekane kama ya upendeleo, unatakiwa kuitendea haki,” anasema Katibu Mkuu huyo Kiongozi.

Anasema; “Usifanye kazi kwa ajili ya kuonwa kama wewe ni mtendaji, fanya majukumu yako kwa kuzingatia weledi, kisha hayo ya kuteuliwa kushika nafasi fulani itakuja yenyewe tu. “Nafasi yoyote unayopewa itendee haki, tenda bila kuwa na matarajio ya kuonwa ili uteuliwe, tumia miongozo na taratibu za sehemu husika zikusaidie kutekeleza kazi yako wa kufuata sheria na miongozo ya mahali pako pa kazi.”

Kumnyima fursa mwanamke kisa maumbile

Baadhi ya wanawake wamesikika wakilalamikia kunyimwa nafasi kwa madai ya jinsia.

Lakini Zena anasema hii si haki. “Usimnyime kazi kwa sababu tu ni mwanamke.” Anasema wapo baadhi ya waajiri bila sababu za msingi, hufikia hatua ya kumnyima mwanamke nafasi ya kazi ama cheo kwa sababu tu ni mwanamke. Zena anasema mwanamke hapaswi kunyimwa kazi au kunyanyaswa kwa sababu za kibaiolojia kwa sababu hakujiumba.

Zena Said afichua siri safari yake ya uongozi

Anatoa mfano kwamba; “Kuna kipindi mwanamke anatakiwa kuwa kwenye likizo ya uzazi, atakuwa na watoto, kwa hiyo anaweza kuwa analea muda unapofika asinyimwe fursa kwa kutumia vigezo hivyo, ni haki yake kama anao uwezo na vigezo vyote, apewe fursa hiyo achape kazi.”

Lakini pamoja na hayo, kiongozi huyo anasema wanawake nao si jambo la busara kutumia fursa hiyo kutaka mteremko au kukwamisha kazi kwa sababu eti ni mwanamke. “Kazi zinakwama kwa sababu ya u -mwanamke wako hili nalo hapana, lazima tuwajibike ipasavyo kama tunavyopaswa kutenda kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi.

Kazi za ofisini na nyumbani

Mwananchi lilitaka kujua, anamudu vipi majukumu ya ofisini na nyumbani. Zena anasema: “Kwa sababu nimempata mwanaume mwelewa sana, hii ni rahisi kwanga kwa sababu ananisaidia sana na kunifanya nipange majukumu yangu ya ofisini na nyumbani kwa wepesi, jambo linalonipa faraja kubwa.” Anasema lengo lake na mumewe ni kutengeneza umoja na mshikamano ndani ya familia yao.

Zena Said afichua siri safari yake ya uongozi

Kauli yake kwa wanaume wanaowakataza wake zao kufanya kazi

Anasema upo mfumo dume kwa baadhi ya wanaume kutokubali wake zao wafanye kazi au kugombea nafasi za uongozi za kisiasa. “Mwanaume aridhie nyumbani kuwe na msaidizi, wapo wanaume wanaokataa kwamba hata chakula kikipikwa na msaidizi nyumbani basi yeye hali, lakini mkishauriana na kukubaliana mkaweka misingi ya kifamilia, mtaepuka mengi na mtasonga mbele.”

Ndoto ya kuwa kiongozi

Kila mtu kwenye maisha ana ndoto zake, leo hii ukikutana na mtoto ukamuuliza kuwa anasoma ili aje kuwa nani? Bila shaka haya ni miongoni mwa majibu utakayokumbana nayo kwa mtoto huyo; nataka baadaye niwe daktari, mwingine mwalimu, polisi, muuguzi na nyingine nyingi.

Hata hivyo, majibu ya swali hilo yaliyotolewa na Zena ni tofauti.

Anasema kipindi anasoma kwa ngazi tofauti, hakuwahi kuwa na ndoto za kuja kuwa kiongozi mwenye dhamana kubwa Serikalini.

Mhandisi Zena anasema alitaka asome kwa lengo la kuja kulipwa mshahara kwa kazi yoyote ile, ambao utakidhi mahitaji yake na ya familia yao nyumbani kwa wazazi wake.

Lakini anasema mambo yalianza kubadilika baada ya kutakiwa kwenda kusomea taaluma ya uhandisi ambayo hata hivyo, hakuwahi kufahamu kabla kama kuna taaluma hiyo.

Anasema aliifahamu baada ya taasisi moja ambayo hakuitaja jina, ilikuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wanaotaka kusoma elimu ya juu, lakini sharti lilikuwa kusomea masomo ya sayansi, hivyo baada ya kuona fursa hiyo, akaomba mkopo huo ambao yeye anauita ulikuwa wa ‘lazima’ na akafanikiwa kuhitimu vizuri.

Kutoka kwenye uhandisi hadi katibu mkuu Ikulu

Zena anasema; “Sikuwahi kujua ipo siku nitakuwa kiongozi, lakini safari yangu imeanzia pale nilipoteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga na baadaye Rais John Magufuli akaniteua kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati. Na baadaye, Rais Dk Hussein Ali Mwinyi akaniona na kuniteua kwa wadhifa huu nilionao.”

Safari yake ya uongozi

Alianza kufanya kazi Ofisi ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), mwaka 2002, na mwaka 2012 akawa mkuu wa kitengo cha masuala ya ununuzi Tanroads makao makuu Jijini Dar es Salaam.

Aprili, 2016 nyota yake ikaanza kung’ara baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa katibu tawala wa mkoa wa Tanga.


Alipokeaje teuzi hizo

Watu wanapoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali huwa wanafurahi hata wengine kufanya sherehe, lakini kwa Zena anasema aligubikwa na hofu ya atatekelezaje majukumu hayo. Anasema aliogopa kwa sababu hakuwahi kushika wadhifa wowote katika ngazi ya utawala na hata nafasi aliyokuwa nayo Tanroadas ilikuwa ni ya utendaji. “Sikuwahi kuwa na uzoefu wa kazi ya utawala, niliogopa sana lakini nikajipa moyo,” anasema Zena. Anasema anamshukuru sana katibu mukhutasi wake (hakumtaja jina) kwa kipindi hicho ambaye anasema alimsaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yake. “Katibu mukhutasi wangu alinisaidia sana, mambo mengi nilikuwa nikimuuliza akawa ananielekeza, ikawa ndiyo faraja kwangu.” Hata hivyo, anasema jambo kubwa lililomsaidia alipoteuliwa kuwa RAS Tanga, alipokea uteuzi huo na akaenda kuifanya kazi hiyo kwa moyo thabiti wa kutaka kujifunza mambo. Lakini pia anamtaja Martini Shigela (Mkuu wa mkoa wa Tanga) kuwa ni miongoni mwa watu waliomsaidia kwa kiwango kikubwa. Anasema baada ya kuitumikia nafasi ya RAS kwa miaka mitatu mfululizo mkoani Tanga, na baadaye kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, aliona kazi sasa inakuwa nyepesi kwa sababu tayari alikuwa amejifunza mambo mengi.

“Pia nilimtanguliza Mungu kwa kila hatua niliyokuwa naipitia,” anasema Zena. Licha ya kukiri kwamba hakuna kazi nyepesi, lakini anasema inaweza kuwa rahisi iwapo mtu akiwa na moyo wa kujifunza mambo mengi anapopata muda.

Anasema hakuna anayejua kila kitu, lakini pia hakuna asiyejua kila kitu, kikubwa ni kujenga imani, utayari wakujifunza mambo mapya kila siku na kutomdharau mtu aliyepo chini yake. “Mimi wakati nateuliwa kuwa katibu tawala ningeweza kusema katibu mukhutasi wangu atanielekeza nini, mimi bosi wake, lakini haikuwa hivyo, yeye alikuwa mwanga kwangu,. Anatoa wito kwa umma kuwa; “hakuna mtu anayeshindwa kufanya kazi, bali unachotakiwa ni kutojifanya mjuaji wa mambo, maana utaharibu.”