Zitto ataja maeneo 10 ripoti ya CAG akitaka Serikali ichukue hatua za haraka

Zitto ataja maeneo 10 ripoti ya CAG akitaka Serikali ichukue hatua za haraka

Muktasari:

  • Zitto achambua masuala 10 katika ripoti ya CAG pamoja na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kuhusu mambo hayo.


Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amechambua na kuainisha maendeo 10 katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku akiitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
 
Zitto amefanya uchambuzi huo leo Jumpili, Aprili 11, 2021 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ambapo pia amegusia makusanyo ya kodi yapo chini, huku akitaka fedha zote zilizochukuliwa na DPP kutokana na kesi za mbalimbali zirejeshwe. 

Pia amegusia madai ya wazabuni dhidi ya Serikali yaliyofikia Sh3.1trilioni, huku akisema Sh2.2 trilioni hazikupita Mfuko Mkuu wa Hazina na Hivyo kutoidhinishwa na CAG matumizi yake.

“Tunashauri CAG afanye ukaguzi Maalumu wa Miradi yote mikubwa inayotekelezwa na Mamlaka ya Bandari ili kupata uhalisia wa ubadhirifu katika TPA. Wakati ukaguzi huo unafanyika tunapendekeza kuwa Mamlaka za Uteuzi zivunje Bodi ya Bandari na kuiunda upya ili kuweza kuweka misingi ya uwajibikaji katika Shirika,” amesema Zitto
  
Mbali na TPA, Zitto ameshauri kukaguliwa zaidi kwa ununuzi wa ndege, kubadili muundo wa uendeshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili kupunguza hasara na utekelezaji mradi wa reli ya kisasa na bwawa la kufufua umeme la Mwalimu Nyerere.
 
Katika  uchambuzi wake Zitto amesema ripoti ya CAG imebaini kwamba, uwezo wa Serikali kukusanya mapato kulinganisha na pato la taifa bado upo chini na kwamba  hali hiyo inasababisha kushindwa kutekeleza Bajeti na kuathiri utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
 
“Suala hili tumekuwa tunalizungumza kila mwaka tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani. Duniani kote ufanisi wa Taifa kukusanya kodi hupimwa kwa kutazama uwiano wa makusanyo ya kodi kwa thamani ya shughuli za uchumi katika nchi husika,” amesema Zitto.
 
Hata hivyo, Zitto amependekeza kuwa Serikali ijielekeze kwenye kuongeza shughuli za uchumi wa wananchi ili kuongeza kipato chao na hatimaye makusanyo ya Serikali.
 
“Serikali iongozwe na filosofia kuwa katika kila kampuni inayoanzishwa na kupata faida Serikali inapata 30% ya hiyo faida,” amesema Zitto.