Zitto ataka Bunge kuondoa sintofahamu uwekezaji bandari Dar

What you need to know:
Chama cha Act Wazalendo kimelitaka Bunge kutanguliza maslahi ya taifa katika mjadala unaotarajiwa kufanyika bungeni Juni 10, 2023 kuhusu uendeshaji wa bandari kadhaa nchini ikiwemo bandari ya Dar es Salaam kati ya serikali ya Tanzania na ile ya Dubai.
Musoma. Chama cha cha ACT Wazalendo kimelitaka Bunge kutanguliza maslahi ya taifa katika mjadala unaotarajiwa kufanyika bungeni Juni10, 2023 kuhusu uendeshaji wa bandari kadhaa nchini ikiwemo bandari ya Dar es Salaam kati ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai.
Hayo yamesemwa mjini Musoma leo Juni 8, 2023 na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alipokuwa akihutubia wakazi wa mji huo kwenye mkutano wa hadhara.
“Hivi karibuni kumekuwepo na mjadala mkali kuhusu suala hili na kwa hakika kumekuwepo na mkanganyiko mkubwa sana ambao pia umeibua hisia kali kiasi cha kupeleka watu kutumia maneno makali na kuvuka mipaka kwani ni maneno ya kibaguzi na ni hatari kwa nchi yetu,”amesema Kabwe
Amesema suala la bandari sio la biashara peke yake bali ni suala la ulinzi na usalama wa nchi kwasababu bandari ni mpaka wa nchi hivyo wabunge wanatakiwa kuhakikisha kuwa suala hilo linapata ufumbuzi wenye maslahi ya nchi.
“Suala la kuuzwa kwa bandari, maeneo ya makubaliano, kuvunjwa mkataba pale pande mbili zikishindana, umiliki wa kampuni ya uendeshaji kama itakuwa hisa sawa kwa sawa, ulinzi wa bandari kama vyombo vya Tanzania ndivyo pekee vitakuwa na jukumu hilo, eneo lipi litaendeshwa na kampuni binafsi na bandari zipi zitakuwa sehemu ya uwekezaji huu, haya yote yanatakiwa kufabyiwa kazi na Bunge letu,”mesema
Amewataka viongozi wa kisiasa kuwa makini na kauli zao kwani zinaweza kuongeza taharuki kwenye masuala ambayo kwa hakika yanahitaji ukweli kuliko hisia.
Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mara, Charles Mwera amewataka wakazi wa mkoa huo kujiunga na chama hicho akidai ndicho kitaleta suluhu kuhusu changamoto zilizopo kwenye jamii na nchini kwa ujumla.
“Malalamiko ni mengi mfano kwenye elimu idadi ya walimu haitoshi watoto wamejaa lakini walimu hawapo na hii ni kwasa babu hao viongozi hakuna watoto wao wanasoma huko ndio maana hawajali sasa njooni huku ACT Wazalendo kwa maslahi ya wote,”amesema
Katibu wa chama hicho mkoa wa Mara, Karume Mgunda amesema kwa hali ilivyo nchini lazima watu wakubali kufanya mabadiliko ili waweze kuondokana na changamoto zilizopo.
"Waliandikisha kaya maskini ili ziweze kusaidiwa kupitia mradi wa Tasaf lakini badala yake hao maskini wamebadilika kuwa trekta wanalima barabara na miradi mingine, unakuta mzee anafanyishwa kazi eti Tasaf hivi hapo wanawasaidia au wanazidi kuwaumiza,”amesema