Zitto kuzindua kampeni za ACT-Wazalendo jimbo la Muhambwe

Tuesday April 06 2021
zittopic

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe

Kibondo. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kesho Jumatano Aprili 7, 2021 atazindua kampeni za chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma.

Katika uzinduzi huo, Zitto atamnadi mgombea wa chama hicho, Julias Masabo. Uchaguzi huo utakaofanyika Mei 2, 2021 unatokana na kifo cha mbunge wa CCM, Atashasta Nditiye kilichotokea Februari 12, 2021 mkoani Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Aprili 6, 2021 katibu mkuu wa chama hicho Wilaya ya Kibondo, Sixbath Bunyambo amesema maandalizi yote yamekamilika huku akiwaomba wapigakura kumchagua Masabo.

Naye msimamizi wa uchaguzi Muhambwe, Diocles Lutema amewataka wadau na vyama vya siasa kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi.

Mbali na ACT-Wazalendo, wagombea wengine wanaoshiriki uchaguzi huo ni Frolence Samizi (CCM) na Bernard Ngarama wa DP. CCM kitazindua kampeni zake Aprili 10, 2021.


Advertisement
Advertisement