Magonjwa ya zinaa yakishika kasi, unyanyapaa kizingiti

Muktasari:

  • Magonjwa ya zinaa yanatajwa kuongeza hatari ya ugumba, matatizo ya ujauzito, saratani, maambukizi ya VVU na Ukimwi.
  • Miongoni mwa magonjwa hayo, kaswende inawaathiri wengi kutokana na takwimu zilizokusanywa katika maeneo ya utoaji huduma za afya.

Dar/Mikoani. Magonjwa ya zinaa yanatajwa kuongeza hatari ya ugumba, matatizo ya ujauzito, saratani, maambukizi ya VVU na Ukimwi.

Miongoni mwa magonjwa hayo, kaswende inawaathiri wengi kutokana na takwimu zilizokusanywa katika maeneo ya utoaji huduma za afya.

Mpango mkakati wa nne wa VVU na Ukimwi katika sekta ya afya wa mwaka 2017-2022 unaonyesha idadi ya waliohudhuria vituo vya afya na kupima kaswende inaongezeka kutoka 878,239 sawa na asilimia 42 mwaka 2017 hadi 1,694,620 (asilimia 73) mwaka 2019.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo, katika mahojiano na Mwananchi amesema idadi ya waliopimwa na kubainika kuwa na kaswende ilipanda kutoka 16,015 mwaka 2017 hadi 26,592 mwaka 2019.

Amesema kaswende, miongoni mwa wajawazito waliopimwa na kupata matibabu, idadi iliongezeka kutoka 10,049 hadi 18,298 katika kipindi hicho.

Profesa Rugajjo amesema jitihada za makusudi zitawekwa kwa kuwa takwimu za matibabu ya kaswende miongoni mwa wanawake waliogunduliwa wanaohudhuria kliniki, ilikuwa asilimia 17.3, 22.4 na 25 katika mikoa ya Tanga, Dodoma na Dar es Salaam na 100 katika mikoa ya Kagera, Geita, Mara na Simiyu.

Hata hivyo, amesema bado uelewa ni mdogo kwa jamii juu ya magonjwa ya zinaa, huku vijana wakiwa katika hatari kubwa.

Amesema upimaji na matibabu ya magonjwa ya zinaa upo kwa kiwango cha chini, huku kukiwa na unyanyapaa. Baadhi ya wagonjwa huzikwepa hospitali na kuishia kupata huduma kwenye famasi.

Serikali imekuwa ikisisitiza kuhusu ngono salama, yakiwamo matumizi ya kondomu ili kujikinga na maambukizi ya maradhi hayo, mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya VVU.

Kwa upande wake, Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza huduma za magonjwa ya zinaa ziunganishwe na za kuzuia maambukizi ya VVU na homa ya ini.

Mtazamo kiimani
Serikali ikihamasisha hayo, viongozi wa dini wanasisitiza jamii kuwa na hofu ya Mungu na kusimamia misingi inayowataka kuepuka zinaa.

Dk Chobo Steve, Mkurugenzi wa Huduma za Jamii na Mkuu wa Idara ya Afya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), anasema jamii na hasa vijana hawana hofu ya Mungu, akisisitiza waishi kwa kufuata amri za Mungu.

“Tunapaswa kuwakumbusha vijana kumpa Mungu nafasi ya kwanza kwenye maisha yao,” anasema Dk Chobo.

Sheikh Khamis Mataka, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na Msemaji wa baraza hilo, amesema vijana wanatakiwa kutoingia katika mahusiano ya kingono kabla ya ndoa.

“Kama aliweza kabla ya ndoa maana yake bado anaweza kuwa na uhusiano na mtu mwingine baada ya ndoa. Hiyo inavunja misingi ya kuaminiana, pia ni tendo linalotengeneza watoto wa nje ya ndoa ambao hukosa baraka au kuwa sehemu ya mifano mibaya inayotengenezwa katika jamii,” anasema.

Hali ilivyo
Wakati Serikali ikihamasisha jamii kutumia kondomu kama mojawapo ya njia za kujikinga na maradhi, yakiwamo ya zinaa; bado hazitumiki ipasavyo na upatikanaji wake kwa baadhi ya maeneo ni wa shida kwa zile zinazotolewa bure.

“Niliwahi kupata ugonjwa wa zinaa, nikaenda duka la dawa nikashauriwa kwenda hospitali. Nilihofia unyanyapaa nikamuomba anisaidie dawa, alinipa,” anasimulia binti wa miaka 22, mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Anasema hakupona, hivyo alilazimika kwenda hospitali alikotibiwa na kupona kabisa.

Dereva wa bajaji katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Michael Simbeye anasema anafahamu matumizi ya kondomu lakini hayazingatii.

Mkazi wa kijiji cha Nsanzya kilichopo Kata ya Kamsamba wilayani Momba, mkoani Songwe, Living Kalengo (20) anasema licha ya Serikali kuzigawa bure, hazipatikani na baadhi huwauzia kwa Sh500 kwenye maduka ya dawa.

Selina (21), mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Dar es Salaam anasema amekuwa na uhusiano na wanaume tofauti hivyo kujiweka katika hatari ya kupata maradhi ya zinaa na mengine ya kuambukiza kwa njia ya ngono.

Pia wapo baadhi ya wasichana wanaojihusisha na biashara ya kujiuza, kama vile ilivyobainika mjini Tunduma, mkoani Songwe.

Kutokana na mwingiliano wa shughuli katika eneo hilo la mpakani mwa Tanzania na Zambia, wapo wasichana wanaojikimu kimaisha kutokana na utaratibu huo unaoweka rehani maisha yao.

Baadhi yao wanasema wanafahamu matumizi ya kondomu lakini miongoni mwa wateja wao hawako tayari kuzitumia.


Uhaba wa elimu
Uhaba wa elimu ya afya ya uzazi unatajwa kuchangia matumizi hafifu ya kondomu.

“Miaka ya 2000 mwanzoni kulikuwa na filamu zilizoonyeshwa vijijini kuhamasisha matumizi ya kondomu, kwenye redio na televisheni pia kulikuwa na matangazo mbalimbali ambayo sasa hayapo,” amesema Amina Ally (52) mkazi wa jijini Dodoma.

Martha Salehe, mwelimishaji rika katika Wilaya ya Ushetu amesema, “Huwa nawaelimisha vijana, hufuata kondomu hospitalini na kuja kuwagawia bure. Wengine wakihitaji hunifuata, ingawa awali waliona kama ni uhuni.”

Kwa upande wake, mwelimishaji rika kwa vijana, Godlove Isdory anasema baadhi ya vijana hawatumii kinga na wanapopata magonjwa ya zinaa huishia kwenda kujitibu kwa kununua dawa famasi.

Amesema yafaa vijana wapewe elimu sahihi kuhusu matumizi ya kondomu na kwamba, hilo lisionekane kuwa jambo lililopitwa na wakati.

Naye Lilian Lema, anayetengeneza maudhui ya afya ya uzazi mtandaoni, amesema matumizi ya kinga yamepungua kwa vijana kutokana na fikra potofu au kutokuwa na elimu sahihi ya umuhimu wake.

Amesema baadhi ya vijana hupeana taarifa potofu kuhusu matumizi ya kondomu na wengine wana taarifa sahihi lakini hupuuzia kuzitumia.

Anatoa wito kwa jamii na wamiliki wa sehemu za starehe, zikiwamo nyumba za kulala wageni na hoteli kuzisambaza vyumbani.

Maduka binafsi
Mhudumu wa famasi katika stendi kuu ya mabasi jijini Mbeya, Atuganile Ambrose anasema wateja wa kondomu wamepungua.

Amesema awali aliuza pakiti kubwa nne kwa wiki moja, lakini miaka ya 2019 hadi 2023 anaishia kuuza moja kwa mwezi mzima.

“Hapa tuna za wanawake pia, lakini zinazouzika zaidi ni za wanaume. Hatuwezi kufanya ulinganifu lakini wateja si wengi kama vile tunavyotarajia,” amesema Emmanuel Shayo, mhudumu wa famasi iliyopo katikati ya Jiji la Dodoma.

Usambazaji
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Dk Saumu Kumbisaga, amesema wamekuwa wakisambaza kondomu maeneo hatarishi kama vile kumbi za starehe na nyumba za kulala wageni.

Dk Saumu amesema magonjwa ya zinaa yapo kwa kiasi kikubwa kutokana na mwingiliano na shughuli za kiuchumi zilizopo.

Ofisa Kinga wa Shirika la Tumaini lililopo Kyela, Ayubu Mwingira, amesema kwa kushirikiana na Serikali wanatoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana.

Mratibu wa shughuli za Ukimwi katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Dk Jackson Kalumula amesema eneo hilo lina changamoto kubwa kutokana na mwingiliano wa watu.

“Kwa wastani, robo mwaka tunasambaza kondomu 75,000 na kwa mwaka ni 300,000,” amesema.

Usambazaji pia hufanyika vijijini kama alivyosema mratibu wa Ukimwi na kinga wilayani Momba mkoani Songwe, Haroub Almassy. Amesema kwa mwaka husambaza kondomu 100,090.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Boniface Kasululu amesema licha ya usambazaji kufanyika, changamoto iliyopo ni kwamba, wanaume ndio waamuzi wa kuzitumia au la.

“Kwa kipindi cha miezi 10 tumesambaza kondomu 400,027, hatuna changamoto kubwa iliyoripotiwa kwa watu kutotaka kuzitumia,” amesema.

Dk Kasululu amesema Songwe ni miongoni mwa mikoa inayopitiwa na barabara kuu iendayo Zambia, hivyo kuwa na maeneo yenye viashiria vya maambukizi ya VVU na hasa Tunduma.

Licha ya kuwapo mpango wa Serikali kugawa kondomu bure katika baadhi ya maeneo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini haziwekwi, huku vitendanishi (Kondomu ATM) zilizowekwa kwenye maliwato, mapokezi kwenye nyumba za kulala wageni zikiwa tupu.

Katika baadhi ya maeneo, kama vile nyumba ya wageni iliyopo katikati ya mji wa Simiyu, zimebadilishwa matumizi na kutumika kuhifadhi risiti, funguo na chaja.

Bohari ya Dawa
Kwa mujibu wa Bohari ya Dawa (MSD), kondomu zimekuwa zikitolewa kwa miradi misonge, hivyo hugawiwa bure.

Meneja wa miradi msonge wa MSD, Elias Katani amesema huwa wananunua moja kwa moja kutoka kwa mtengenezaji.

“Anayetuuzia sasa yuko India, huyu ndiye tuliyeingia naye mkataba wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka huu wa 2023,” amesema.

Amesema kupitia programu ya kudhibiti Ukimwi chini ya Wizara ya Afya, walisaini mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani 9.2 milioni, sawa na Sh23.049 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa kondomu.

Amesema zilizopo ni 516,963 (kwa ujazo wa pakiti 100 kila moja) na kwa mwezi huombwa 74,860.

Katani amesema zilizopo zilipokewa Septemba 30, mwaka huu zikiwa sawa na asilimia 42 ya mahitaji yote ya kondomu zilizoombwa.

“Ukiangalia idadi ya kondomu zilizosambazwa na zilizopokewa, tuna kondomu za kutosha zinazoweza kutupeleka mwaka mmoja na zaidi,” amesema.

Kuhusu uhakiki wa ubora, amesema Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) hufanya kazi hiyo na baada ya kujiridhisha ndipo husambazwa.

Mchunguzi wa vifaatiba na vitendanishi wa TMDA, Samson Mwambene alisema uchunguzi hufanyika kupitia mashine maalumu yenye uwezo wa kubaini hata vishimo vidogo iwapo vipo katika kondomu.

“Mashine hii ina uwezo wa kubaini hitilafu ambazo huwezi kuziona kwa macho kama kuna tundu lolote. Si lazima iwe ilitengenezwa chini ya ubora, lakini kuna uwezekano ikatokea changamoto katika uzalishaji zikapata matundu au kwenye usafirishaji imesafirishwa kwenye hali ya joto kubwa au unyevu,” amesema.

Katani amesema kondomu husambazwa kwa wingi zaidi katika kanda za Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam, kutokana na wingi wa watu na maeneo.

Amesema muda wa matumizi ya kondomu ni miaka mitano tangu kutoka kiwandani.

Uzalishaji nchini
Miaka miwili imepita tangu Tanzania iingie katika mchakato wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha glavu, ambacho pia kinatarajiwa kuzalisha kondomu.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema, “Kama unazalisha glavu ni rahisi pia kuzalisha kondomu. Kwa hiyo, mpango uliopo tulishaimarisha uzalishaji wa glavu ambao ulikuwa wa majaribio baada ya kuibuka janga la Uviko 19,” amesema.

Amesema, “Tukiweza kuzalisha hizi za kutosha, moja ya eneo tunaloliona la soko la wazi ni uzalishaji wa kondomu na tunaweza kuwa na kiwanda kinachozalisha bidhaa hizi.”
amesema kampuni tanzu imeundwa kwa ajili ya uzalishaji. 

“Kampuni hii ina uwezo wa kuingia makubaliano na nyingine. Kwa mfano, kiwanda hikihiki kinachotuuzia sasa kina uwezo wa kuingia ubia na kampuni tanzu hii kuzalisha kondomu na kuzisambaza,” amesema.

Imeandikwa kwa ushirikiano wa Bill $ Melinda Gates Foundation