Zingatia haya kabla hujamshika mtoto mchanga
Dar es Salaam. Mtoto anapozaliwa ni furaha, hasa katika maisha ya mwanamke pale wakati sahihi unapowadia.
Siyo kwa mama na baba pekee bali pia hata wazazi, familia pamoja na jamii inayomzunguka zinapowafikia taarifa za kuzaliwa kwa mtoto akiwa salama yeye pamoja na mama yake.
Anaporuhusiwa mama na mtoto kutoka hospitali ndugu, jamaa na marafiki hujawa na shauku ya kutaka kuwaona na kutoa pongezi kwa mama.
Pamoja na furaha hiyo walio wengi hawajui nini hupaswa kuzingatia kabla ya kumtembelea mama aliyejifungua na kumshika mtoto. Hali hii husababisha baadhi yao kuondoka wakimwachia maradhi ya mafua, ngozi mtoto mchanga.
Clara Joseph ambaye ni mama wa mtoto wa miezi sita anasema alipojifungua alipata faraja kuona ndugu zake wakienda kumuona yeye na mtoto wake, japokuwa ilikuwa inamfanya kushindwa kupumzika ipasavyo.
“Ninapokuwa nimepumzika anapotokea mgeni inabidi nikazungumze nae hadi atakapoondoka ndio nipumzike tena, ilikuwa inanipa faraja japokuwa ilinifanya kutopata muda wa kutosha kupumzika,” anasema.
Ashura Mohammed anasema yeye anajiskia fahari kuona watu wengi wakimtembelea kwa nia ya kumuona baada ya kujifungua.
Hata hivyo wataalam wa afya wanashauri kuzingatiwa kwa mambo kadhaa, ili kuwafanya mama na mtoto kubaki salama.
Akizungumza na Mwananchi Ofisa Mkunga Msaidizi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga anasema kwa kuwa imezoeleka katika jamii mama anapojifungua ndugu, jamaa na marafiki huenda kuwaona na kuwapongeza ni muhimu kuepuka lazima ya kila mgeni anaekuja kumshika mtoto.
Mganga anasema hivyo kwa sababu mtoto anapozaliwa kinga yake inakuwa haijaimarika vizuri, hivyo kwa kipindi hicho ni rahisi kuambukizwa magonjwa kama vile mafua, kuhara pamoja na kikohozi.
“Pia baadhi ya wageni wanaokuja wanaweza kuwa wamejipaka manukato yenye harufu kali yanaweza kuleta athari kwa mtoto, hivyo kwa kipindi hicho ni muhimu kupunguza mgusano wa mtoto na watu wengine, itoshe kumsalimia mama na kumpatia zawadi kisha ukaondoka,” anasema.
Anasema kama ina ulazima wa mtu huyo kumshika mtoto ni muhimu kuzingatia kutotumia manukato yenye harufu kali, pamoja na usafi wa mwili ikiwemo mikono yake kabla ya kufanya hivyo.
“Ni vyema kuhakikisha ananawa mikono yake vizuri na ikiwezekana ajifunike nguo kama vile kanga, kitenge au kitambaa safi kisichokuwa na harufu ndipo aweze kumshika mtoto, itasaidia kupunguza mtoto kupata bakteria na virusi ambavyo vinaweza kusababisha apate magonjwa,” anasema.
Vilevile anahimiza mtu anapokwenda kumuona mtoto mchanga kuepuka tabia ya kuwashikisha fedha mikononi, kuwashika shika watoto maeneo ya usoni na mikononi.
Kutumia muda mfupi
Pia anasema ni muhimu kwa wanaokwenda kumtembelea mama aliyetoka kujifungua kuhakikisha wanatumia muda mfupi kuzungumza na mama, ili apate muda wa kutosha wa kupumzika.
Anasema mama anapojifungua yeye na mtoto wanatakiwa kupata muda wa kutosha kupumzika na kuwa sambamba na mtoto wake
Hiyo inamfanya mama aweze kumnyonyesha mtoto wake mara kwa mara, jambo linalochochea mama kuzalisha maziwa ya kutosha na mtoto kupata virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji wake.
“Mama anapotoka kujifungua anakuwa amechoka, pia wakati mwingine huweza kupata msongo wa mawazo kutokana na masuala mapya ya kuwa mama na malezi, hivyo huhitaji muda wa kutosha ili aweze kupata nguvu za kumhudumia mtoto ipasavyo,” anasema.
Kupunguza ushauri
Mganga pia amehimiza wanaokwenda kumtembelelea mama aliyetoka kujifungua kuacha tabia ya kuwakatisha tamaa, haswa katika kufuata ushauri waliopewa na wataalamu wa afya.
Ametolea mfano katika upande wa unyonyeshaji anasema baadhi ya watu wamekuwa wakiwakatisha tamaa baadhi ya wanawake waliotoka kujifungua kuwa kumpa mtoto maziwa ya mama pekee, hawezi hashibi hivyo kumshauri kumpa uji mwepesi pamoja na maji.
“Hayo yanamfanya mama kukata tamaa katika safari yake ya unyonyeshaji, waacheni wafuate ushauri wanaolekezwa na wataalam wa afya,” anasema.
Epuka maneno yatakayompa msongo wa mawazo
Anasema ni muhimu mtu anapokwenda kumuona mama aliyetoka kujifungua, kuacha kuongea maneno yatakayosabisha kumpa mama msongo wa mawazo.
Anatolea mfano kumwambia mama kama amenenepa, kupungua sana au kubadilika muonekano wake kwa ujumla.
“Kumbuka mama huyo alikuwa na safari ya miezi tisa akiwa amebeba ujauzito, amepitia mabadiliko mengi ambayo yanahitaji muda ili kurudi katika hali ya kawaida, kumnyoshea vidole na kumwambia maneno hayo yatamvunja moyo,” anasema Mganga.
Pia anahimiza baadhi ya watu kuacha tabia ya mtoto anapokuwa mchanga kuhoji mbona hajafanana na wazazi au ndugu zake wa karibu.
“Mama anapotoka kujifungua, akipata msongo wa mawazo kwa namna yeyote ile huathiri utokaji wa maziwa mengi na yenye ubora,” anaeleza.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Masuala ya Chakula na Lishe na Meneja mradi wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daud Gambo anaongeza kuwa kwa mtu ambaye anajihisi kwa wakati huo kuwa na magonjwa kama vile mafua, homa na kikohozi ni vyema kuepuka kumtembelea mama aliyetoka kujifungua hadi pale atakapopona kabisa ili kumkinga mtoto na maambukizi.
Anaongeza kuwa ni vyema wanapokwenda kuwaona kuwabebea zawadi, kumpa mama maneno ya faraja na kumpongeza.