Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mifumo ya utakatishaji fedha na jinzi unavyoathiri uchumi

Muktasari:

Hili ni kosa la jinai ambalo wahusika wakitiwa mbaroni hushtakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji ya mwaka 2006 na wahusika wakitiwa hatiani huadhibiwa vikali ikiwa ni pamoja na utaifishaji wa mali na kufungwa jela.

Wahalifu  wanapoiba kiwango kikubwa cha fedha  au mali hujaribu kutafuta namna ya kuzihalalisha ili zionekane ni mali halali ambayo mtu au vyombo vya dola haviwezi kuhoji juu ya upatikanaji wake. Hii ni njia inayofanyika ili kuficha ukweli wa uhalifu uliotendeka.

Hili ni kosa la jinai ambalo wahusika wakitiwa mbaroni hushtakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji ya mwaka 2006 na wahusika wakitiwa hatiani huadhibiwa vikali ikiwa ni pamoja na utaifishaji wa mali na kufungwa jela.

Wizara ya Fedha, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), inaelezea suala la utakatishaji fedha kuwa ni shughuli au vitendo vyenye lengo la kuficha ukweli au asili ya fedha au mali iliyopatikana kutokana na uhalifu.

FIU inaeleza kwamba fedha nyingi zinazotakatishwa hutokana na usafirishaji dawa za kulevya, rushwa, usafirishaji binadamu, ukwepaji kodi na njia nyingine za kihalifu na kwamba lengo la watekelezaji wake ni kujaribu kukwepa mkono wa sheria unaosimamiwa na Serikali.

 

Watu wanaopata fedha haramu hutafuta namna ya kuzisafisha kwa kuzipitisha kwenye vyombo vya fedha au kwa kuziwekeza kwenye vitega uchumi.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Uhalifu na Dawa za Kulevya (UNODC) ilifanya utafiti kwa ajili ya kubaini ukubwa wa tatizo la utakatishaji fedha zitokanazo na biashara ya dawa za kulevya.

Katika ripoti hiyo ilibainika kuwa Dola 1.6 trilioni za Marekani sawa na asilimia 3.6 ya pato la dunia kwa mwaka zilitakatishwa.

Kwa mujibu wa UNODC mtakatishaji fedha huanza kwa kuziingiza fedha kwenye mifumo ya kifedha kama vile benki kidogokidogo kisha baadaye huzitoa na kuziingiza kwenye akaunti moja kama fedha halali.

Umoja huo unaeleza kuwa mtakatishaji akishafanikiwa kuvuka hatua ya kwanza, hujaribu kuihamisha kutoka chanzo cha awali na kuiingiza kwenye mifumo mingine ya kifedha ikiwa ni pamoja na kununua hisa.

“Akishafanika hapo, mtakatishaji fedha huenda hatua ya tatu na kujiingiza kwenye ununuzi wa vitega uchumi kama majengo, magari ya kifahari au kufungua kampuni mbalimbali,” inasema taarifa ya UNODC.

Umoja wa mataifa unasema kuwa utakatishaji wa fedha unatokea zaidi katika mataifa ambayo ina mifumo dhaifu ya kusimamia fedha kwa sababu lengo la uhalifu huo ni kumrejeshea mhusika fedha zikiwa safi.

UNODC inaongeza kuwa utakatishaji wa fedha una madhara makubwa kwa taasisi za fedha duniani kwa kuwa umekuwa ukishusha heshima ya benki hizo zinapobainika kutumika kufanikisha uhalifu huo.

“Kama fedha zilizopatikana kwa njia ya uhalifu zinaweza kuingizwa katika taasisi fulani ya fedha kupitia mfanyakazi wa kawaida au wakurugenzi ambao wamepewa rushwa ili wayafumbie macho matendo hayo,” inasema taarifa ya UNODC na kuongeza kuwa madhara ya matukio hayo huiathiri benki husika na wateja wake.

Iwapo vyombo vya fedha hazitadhibiti utakatishaji wa fedha, jamii inaweza kujikuta ikitawaliwa na makundi ya wahalifu ambao wanaweza kushiriki sekta muhimu za kiuchumi kwa njia ya uwekezaji baada ya kutoa rushwa kwa viongozi serikalini.

Kutokana na uhalifu huo kufanywa na watu wenye nguvu kifedha, jamii inapaswa kushirikiana na vyombo vya udhibiti na kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vinakomeshwa kwa faida ya wananchi wote.

FIU inasema: “Utakatishaji fedha unakwamisha nchi kufikia malengo yake ya kitaifa. Kitendo hicho kinaweza kuharibu uamuzi wa kibiashara, kuziyumbisha benki, kuzifanya sera za uchumi kushindwa na kushusha heshima ya nchi.”

Utakasaji wa fedha unaweza kudhoofisha uchumi, siasa na jamii kwa ujumla kwa sababu makundi ya kihalifu yanaweza kujipenyeza kwenye taasisi, kudhibiti kiasi kikubwa cha fedha kupitia uwekezaji kwenye sekta muhimu, kuwahonga viongozi nyeti ndani ya nchi na hatimaye Serikali kuongozwa na wahalifu.

Kutokana na mfumo huo ndiyo kusema Serikali yenye viongozi wadhaifu, wasioweza kukataa rushwa, inaweza kujikuta inaangukia mikononi mwa wahalifu na kuifanya nchi iwe chini ya viongozi wanaowasujudu wahalifu.

Nguvu ya kiuchumi na kisiasa inayotokana na makundi ya kihalifu inaweza kudhoofisha mfumo wa jamii nzima kwa kuharibu maadili na baadaye kuondoa mfumo wa kidemokrasia katika jamii.

Kwa mujibu wa Tume inayoshughulikia Makosa ya Kihalifu kwa Njia ya Fedha na Uchumi (EFCC), watunga sheria na wadau wengine barani Afrika wanatakiwa kuongeza nguvu kupambana na utakatishaji fedha kwa kuwa hadi kufikia Aprili mwaka huu takriban Dola 50 bilioni za Marekani, sawa na Sh1.3 trilioni, zilikuwa zimekwisha takatishwa.

Akizungumza nchini Nigeria hivi karibuni, Mkurugenzi wa Fedha wa EFCC, Bukar Abba anasema utakatishaji fedha ni miongoni mwa makosa mabaya yatakayotokomezwa iwapo jamii itaamua kushirikiana kupiga vita uhalifu huo.

“Fedhi nyingi zimekuwa zikipotea kupitia malipo ya kibiashara, ukwepaji kodi, uharibu wa kitumia utakatishaji fedha, dawa za kulevya na usafirishaji binadamu,” anasema Abba.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Profesa Honest Ngowi anasema utakatishaji fedha haukubaliki katika jamii kwa kuwa chanzo cha fedha hizo ni uhalifu.

Profesa Ngowi anasema kuwa iwapo wahalifu hao wataamua kusafirisha fedha hizo nje ya nchi, wanaweza kukwamisha baadhi ya miradi ya maendeleo kwa kuwa watalazimika kusafirisha kiwango kikubwa cha dola zilizokuwa kwenye mzunguko nchini.

“Utakatishaji fedha una athari kubwa sana kwa mtu mmojammoja kwa kuwa bajeti ya Serikali inaweza kukwama na kukwamisha miradi iliyokusudiwa kutekelezwa,” anasema Profesa Ngowi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju anasema hivi sasa wahalifu wanatumia maendeleo yaliyofikiwa katika teknolojia ya habari na mawasiliano kuzalisha fedha haramu.

“Wahalifu wanatumia fursa iliyoletwa na maendeleo ya mifumo ya mawasiliano na teknolojia katika biashara kutakatisha fedha zinazopatikana kwa njia ya uhalifu na kuzisafirisha haraka katika nchi nyingine ili kuficha uhalisia wa mali hizo na kuepuka kukamatwa na vyombo vya uchunguzi hapa nchini,” anasema Masaju.

Hii inaashiria kuwa wahalifu na mafisadi wanatumia mbinu mbalimbali za kutakatisha fedha, hivyo ni muhimu watawala pamoja na vyombo vya dola kusimama imara kukabili tatizo hili ambalo linaweza kuwa chanzo cha kuangamiza uchumi wa nchi.