Dully Sykes : Kutoka ‘Nyambizi’ mpaka ‘Utamu’ na bado anatisha

Msanii Dully Sykes akiwa katika Studio yake iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Kwa mara nyingine Dully anakutana na Mwananchi Jumamosi akiwa katika Studio yake ya 4.12 (zamani Dhahabu Records) iliyopo maeneo ya Tabata Kimanga, Dar es Salaam na kueleza mengi katika safari yake kimuziki.
Ni miaka 13 sasa amefanikiwa kudumu katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, kipindi ambacho wameibuka wasanii wengi wa muziki huo na kushindwa kuhimili vishindo na kuamua kuachana na sanaa hiyo.
Wakati anaanza muziki huo ilikuwa ngumu, enzi hizo studio kali zilizotamba zilikuwa ni Bongo Records, Mika Mwamba na Mj Records chini ya mkali, Joachim Kimario.
Upinzani ulikuwa mkubwa, wasanii walikuwa wakipishana studio na kumbi mbalimbali za burudani, wakiwa wamebeba mabegi mgongoni yaliyojaa kazi zao mbalimbali, lengo likiwa ama kupata shoo au nyimbo zao kusikia redioni.
Wakati huo wazazi walikuwa wakali, habari za vijana wao kujiingiza katika muziki, kwa wengi zilikuwa zikiwaudhi kuliko jambo lolote lile.
Hapa namzungumzia mkongwe aliyezaliwa na kukulia mitaa ya Kariakoo, Anthon Edward Wayson maarufu kama Dully Sykes ambaye ni mmoja kati ya wasanii wa Bongo fleva wanaotamba na wanaoendelea kutamba. Moja ya sifa kubwa ya msanii huyo ni mmoja wa wasanii walioshirikishwa katika nyimbo nyingi.
Kwa mara nyingine Dully anakutana na Mwananchi Jumamosi akiwa katika Studio yake ya 4.12 (zamani Dhahabu Records) iliyopo maeneo ya Tabata Kimanga, Dar es Salaam na kueleza mengi katika safari yake kimuziki.
Mwananchi Jumamosi: Dully Mambo vipi, Pole na makujuku
Dully: Poa, karibu sana!
Mwananchi Jumamosi: Kuna tofauti yoyote kati ya Dully aliyeimba Nyambizi na huyu anayemtamba wimbo wa Utamu kwa sasa?
Dully: Kuna mabadiliko makubwa sana, kuanzia muziki wangu, kufikiri kwangu na maisha yangu kwa ujumla, kipindi natoa wimbo wa ‘Nyambizi’ sikuwa na uwezo wa kutumia chombo chochote, sikujua kuchagua muziki unaofaa, sikuwa na uwezo wa kuzalisha muziki.
Kwa sasa ninapiga vyombo vyote vya muziki, ni mzalishaji wa muziki, mpaka sasa nimeshiriki kutengeneza nyimbo nyingi tu ikiwemo ya Amen (Mwana FA), Dar Stand Up (Chid Benzi) na nyimbo zangu za Utamu, Joka na Mtoto wa Kariakoo.
Mchango wangu umeongezeka; kwa siku ninaweza kupokea zaidi ya simu 15 za wasanii chipukizi wakihitaji msaada wangu na huwezi kutaja mafanikio ya Diamond, Ommy Dimpoz na wengine wengi bila kumtaja Dully.
Kipimo cha ubora wangu ni pamoja na mialiko katika nchi mbalimbali barani Ulaya na Afrika, kwa sasa nimepata ziara ya kwenda Uingereza, wakati wowote kuanzia nitaondoka nchini kueleka huko na tumekubaliana kuwa watanilipa Paundi 3,500 (Sh8.8milioni) na sitalipia gharama yoyote nikiwa huko. Hayo ni mafanikio na mabadiliko makubwa sana kwangu ukilinganisha na kipindi cha miaka ya nyuma.
Mwananchi Jumamosi: Kwa mara ya mwisho umetoa albamu lini?
Dully: Ilikuwa mwaka 2005 na sitaki kutoa tena albamu nyingine.
Mwananchi Jumamosi:Kwanini?
Dully: Hakuna maslahi yoyote, albamu ni kama biashara ya kuuza mahindi, kwa sababu haiwezekani niuze albamu kwa Sh5milioni, fedha ambazo ninaweza kuingiza kwa siku moja kwenye shoo.
Mwananchi Jumamosi: Pamoja na mafanikio mengi uliofikia bado unaishi na mama yako mzazi, kuna sababu ya kufanya hivyo?
Dully: Nimeamua kuishi karibu na mama kwa sababu bado ninahitaji zaidi malezi yake, ni nguzo ambayo bado natakiwa kuwa nayo karibu, vijana wengi wanapotea kimaisha kwa kukosa msingi na mawazo ya busara kutoka kwa wazazi.
Mwananchi Jumapili: Kama ni nguzo, kauli gani ambayo amekuwa akikwambia kama silaha ya maisha yako?
Dully: Nihakikishe najenga msingi wa maadili na umakini katika maisha ya watoto wangu.
Mwananchi Jumapili: Hao watoto wako wapi kwa sasa?
Dully: Wako watatu ila kila mmoja anaishi na mama yake.
Mwananchi Jumamosi: Una mpango gani juu ya familia yako kwa baadaye au bado upo upo kidogo?
Dully: Hapana kwa sasa ninaye mchumba wangu ambaye tutafunga ndoa miaka miwili ijayo, tumeshapanga na kukubaliana hivyo.
Mwananchi Jumamosi: Pamoja na hilo umekuwa ukibadilisha majina, ulijiita Mr Misifa mara Hadsome na sasa ‘Brazamen’, kwanini inakuwa hivyo?
Dully: Hapana siyo kama nabadilisha majina ila huwa naboresha, lengo ni kukuza soko langu la muziki, ukaribu zaidi na watoto wa kike ni kwa sababu wanakubali sana muziki wangu, ndiyo wateja wangu wakubwa.
Hufanya hivyo kwa maslahi ya kibiashara zaidi na wala siyo kwa ajili ya kustarehe nao.
Mwananchi Jumamosi: Dully kati ya mademu na muziki unapenda ni zaidi?
Dully: Napenda sana muziki, nasema hivyo kwa sababu mimi nautafuta muziki, lakini mademu wananitafuta mimi,na hao mademu wananitafuta kwa sababu wanapenda muziki wangu.
Mwananchi Jumamosi: Tuachane na hayo, naomba unitajie ngoma (nyimbo) zako 20 bora unazozikubali
Dully: Kuna nyimbo za Salome, Nyambizi, Tamika, Joka, Utamu, Historia ya kweli, Mr misifa, Handsome, Asha my promise, Mtoto wa Kariakoo, Dhahabu, Roud spika, Popo, Shikide, Bibelo, Hunifahamu, Julietha, Watasimiliwa, Eva na Hai.
Mwananchi Jumamosi: Kuna wimbo lazima utakuwa mzuri zaidi, ni upi kati ya hizo nyimbo 20?
Dully: Ni ngoma ya Salome, huu wimbo nilitumia akili sana kuandaa. Una thamani kubwa hata ukiilinganisha na Utamu japokuwa Utamu imebamba zaidi mashabiki wangu kuliko zote nyimbo zote kwa sasa.
Mwananchi Jumamosi: Ukiniachia muda wako sitomaliza,kwa leo naomba niishie hapo
Dully: Poa, shukrani sana.