Siri wengi kukimbilia ‘PhD’ za heshima

What you need to know:

Katika mfululizo wa makala hii iliyoanza jana, tuliangazia kwa kina taratibu za usomaji wa shahada ya uzamivu katika vyuo vya Tanzania.

By Abeid Poyo

Katika mfululizo wa makala hii iliyoanza jana, tuliangazia kwa kina taratibu za usomaji wa shahada ya uzamivu katika vyuo vya Tanzania.

Leo makala inaanza na namna vyuo vikuu vinavyojipanga dhidi ya vitendo vya udanganyifu. Mwisho tutaangazia sababu zinazowasukuma baadhi ya watu kujipa usomi wa PhD hata kama hawakupita vyuoni au kutunukiwa shahada za heshima kutoka katika vyuo vinavyotambulika. Endelea...

Katika chapisho la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam liitwalo; ‘Guidelines and regulations for plagiarism and deployment of post graduate students for teaching or technical assistants’, chuo hicho kikongwe nchini kinakiri kuwapo kwa udanganyifu wa kitaaluma hasa ule wa ubwakuzi (plagiarism) wa kazi za wengine.

Chapisho hilo la mwaka 2016, linaeleza kuwa ubwakuzi ni changamoto inayovikabili vyuo vingi duniani, kikiwamo chuo hicho na kwamba hali hiyo chuoni hapo inaonekana kuwa ni tatizo linalokua, hivyo kuhitaji namna ya kulitatua.

Kwa mujibu wa chuo hicho, kosa la ubwakuzi likibainika hatua za kinidhamu huchukuliwa kwa msimamizi na mwanafunzi. Aidha, chuo kinatumia mbinu mbalimbali, zikiwamo za kiteknolojia katika kubaini kama kazi za wanafunzi wake zimebwakuliwa au la.

“Tuna software ya ‘Turnitin’ ambayo ina uwezo wa kubaini originality (uhalisia) wa kazi za kitaaluma... na tangu tuanze kuitumia, ni lazima kazi ya mwanafunzi ipitie software hiyo, ili ijulikane kiwango cha uhalisia wa kazi kiasilimia,’’ alisema Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye katika mahojiano aliyofanya na gazeti dada la The Citizen mwaka 2020.

Aliongeza: “Tukigundua mtu amebwakua mara moja tuna revoke (batilisha) kazi na tumeshawafukuza baadhi ya wanafunzi kwa kughushi.’’

Kwa chuo kikongwe na kinachosifika kwa umakini nchini, kukiri kuwapo kwa tatizo la ubwakuzi ni dalili kuwa katika vyuo vingine hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini vyuo vingi vina sera na sheria ndogondogo zinazosimamia masuala ya ubwakuzi na hatua za kuwachukulia wabwakuaji. Sera na sheria hizo pia zinaenda na matumizi ya tekolojia kama vile ‘Turnitin’ yenye uwezo wa kung’amua kazi zilizofanywa kwa kubwakuliwa.


Siyo Tanzania pekee

Ubwakuzi ni tatizo la kidunia. Katika andiko lake Plagiarism: the cancer of east African university education (Journal of Education and Practice, Vol 4. No 17, 2013), Okoche John anasema kama tatizo hilo halitapewa uangalizi wa karibu, litaendelea kuangamiza elimu ya vyuo vikuu kama ugonjwa wa saratani.

Anasema moja ya mambo yanayochochea hali hiyo ni pamoja na matumizi ya teknolojia, ikiwamo kompyuta na intaneti.

“Intaneti na matumizi ya kompyuta yanawezesha mtu kupata makala, tasnifu na machapisho kutoka duniani kote na haya yanawezekana kwa mtu kuyanakili,’’ anasema.


Undani wa PhD

Uzamivu au udaktari wa falsafa (PhD), ni ngazi ya juu katika mifumo ya kitaaluma kwa vyuo vikuu nyuma ya uprofesa.

Msomi wa fani za lugha na elimu. Sheikh Khamis Mataka anasema ngazi hiyo ni uthibitisho kuwa mhusika amebobea au kuzama katika fani husika.

‘’Udaktari ni uthibitisho wa wewe kuwa mwanazuoni uliyezama kielimu na kitaaluma katika eneo fulani na ndiyo maana inaitwa Shahada ya Uzamivu yaani uthibitisho wa Uzamivu na kwamba wewe ni mwalimu wa kuwafundisha wanafunzi wa vyuo vikuu,’’ anasema.

Duniani kote shahada ya udaktari wa falsafa hutolewa katika sura tatu, ya kwanza ikiwa ni ile ya mwanafunzi kufanya utafiti chini ya uangalizi wa wasimamizi maalumu wa ndani na nje ya chuo. Baada ya utafiti mhusika hulazimika kuandaa tasnifu au tazmili (dissertation/ thesis).

Kwa taasisi kama Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, mwanafunzi anaweza kuchukua miaka kati ya mitatu hadi nane kuhitimu shahada yake.

Aina ya pili inajumuisha tamrini (mazoezi ya darasani), kufanya utafiti na kisha kuandaa tasnifu (course work and dissertation).

Hapa mwanafunzi anatahiniwa darasani kwa alama maalumu na kisha kufanya utafiti ambao pia huwa na alama maalumu. Mchakato wote huhusisha pia wasimamizi/watahini wa ndani na nje ya chuo.

Aina ya tatu mhusika hakai darasani, hafanyi utafiti wala hajiandikishi kama mwanafunzi. Shahada hii ya heshima, hupewa mtu kutokana na mapendekezo ya mkuu wa chuo na baraza la taaluma maarufu kama ‘senate’.

“Hutolewa kutambua, kuheshimu, kuthamini na kuenzi mchango wa mhusika katika maendeleo na ustawi wa jamii,” anafafanua Dk Mohamed Maguo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Naye Profesa Mwandosya anasema kuwa shahada ya heshima ya udaktari hutolewa na vyuo vikuu vyenye ithibati kutambua mchango wa mtu katika maendeleo ya taaluma au ya jamii.

“Kawaida, popote pale unapotunukiwa shahada hiyo, huitwi daktari fulani,’’ aliandika Profesa Mwandosya katika ukurasa wake wa twitter Mei 29, 2021.


Sababu watu kukimbilia PhD ya heshima

Aina hii ya tatu hata hivyo, imekuwa na utata, hasa kutokana na kutamalaki kwa vyuo visivyo na ithibati ndani ya nchi na hata kimataifa, vinavyotoa shahada za heshima hata kwa watu ambao kwa jicho la kawaida hawana sifa stahiki.

Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), shahada hii ya heshima inapaswa kutolewa na vyuo vyenye ithibati kutoka tume na kutambuliwa na sheria ya vyuo vikuu.

Kwa vyuo vikuu vya nje, mwongozo ambao mara kwa mara hutolewa na TCU unaeleza kuwa, lazima viwe vinatambulika na kusajiliwa na mamlaka katika nchi husika.

Watu mbalimbali, akiwamo Mwalimu Julius Nyerere wanasifika kwa kuwa na shahada lukuki za PhD za heshima kutoka vyuo vinavyotambulika kimataifa.

Aghalabu hawakuwa wakijita madaktari kama ilivyo ada hivi sasa kwa baadhi ya watu, hususan wanasiasa na viongozi wa dini, wanaosukumwa kufanya hivyo kwa sababu ya kutaka umaarufu na hadhi.

Kwa mujibu wa Sheikh Mataka, ni ujinga uliotopea wa mtu kujipa hadhi asiyokuwa nayo. Anasema: “Maadili ya kitaalamu yameingiliwa na usomi umekuwa ni majigambo zaidi badala ya kazi za kitaalamu na kitaaluma. Ni uzumbukuku.’’

Ni dhahiri kutokana na mjadala uliopo kuhusu yanayoendelea sasa katika vyuo mbalimbali, TCU inapaswa kuvaa kibwebwe katika kudhibiti mifumo, taratibu na vigezo vya utoaji wa shahada za juu nchini, ili kusiwepo na mianya inayoweza kutumiwa na watu wasio na uwezo kusomea ngazi hiyo nyeti katika mfumo wa elimu nchini.

Kesho tunamaliza mfululizo wa makala hii kwa kuangazia machungu wanayopitia baadhi ya wanafunzi wanaosoma shahada za juu nchini kutoka kwa wasimamizi wao.