ANTi BETTIE: Shoga mbona “unausokotola” unyago, unamtia aibu somo yako

Kwenye ndoa kuna mambo mengi, ikiwamo kupanda na kushuka na changamoto za hapa na pale, ndiyo maana mara nyingi watu husema inahitaji uvumilivu. Pamoja na changamoto hizo, bado ndoa inabaki na sifa yake ileile na wala hakuna haki kwa mwanandoa kulipa kisasi kiasi cha kuishushia hadhi.

Wapo wanandoa wanaojinasibu kwa kuwaonyesha kazi wenza wao, “eti dawa ya jeuri ni kiburi...” hapana ndoa haitaki hivyo.

Kuna mambo mengi yanayowachosha wanaume kutoka kwa wenza wao, ikiwamo dharau, nyodo na kiburi.

Hakuna jambo baya na linalowachosha wanaume kama kujiona wewe ndiyo wewe mbele ya mumeo, ndiyo maana ndoa imehalalishwa kwa mwanamke na mwanamume, hivyo bado ana umuhimu kwako.

Hakuna mwanamke wala mwanamume anayeweza kujioa mwenyewe, hivyo kuna kila haja ya wenza kuthaminiana, kuvumiliana na kuheshimiana.

Malalamiko makubwa kutoka kwa wanaume ni kuwa baadhi yenu mkikaa na waume zenu mnazungumzia mambo makubwa ambayo yapo nje ya uwezo wao, na mnalijua hilo mnafanya makusudi kuwakera.

Hata mkiletewa zawadi mnazilinganisha na walizoletewa wenzenu siku mbili zilizopita... “Rafiki yako juzi katika maadhimisho ya miaka mitatu ya ndoa yao, alimnunulia mkewe Vits...nashukuru na mimi katika maadhimisho ya miaka 12 ya ndoa umeniletea ua...!”

Hii ni dharau na aliyefanyiwa aliniambia, alitamani kujificha kutokana na jinsi alivyokatishwa tamaa.

Si hao tu, wapo wale wanaokataa kutoka na wenza wao kisa hawajanunuliwa nguo mpya. Hiki ni kiburi na dharau ya hali ya juu katika mahusiano na ninachokijua mimi wazazi waliwatafutia masomo wa kuwafunda ili mkawe wake bora na siyo bora wake.

Jamani hata ukiwa mrembo wa sura na umbo, kama huna tabia nzuri utabaki kutolewa mfano mbaya siku zote maishani, hakuna mwanamume anayependa mwanamke anayempanda kichwani.

Inawezekana kuna mahali wenza wenu wanakosea, lakini kumbuka ukiibananga ndoa mwanzoni kwa kuiacha ijiendeshe, ujue mbele ya safari itakutesa

Nyodo, kiburi, dharau havijengi, siku zote vinabomoa. Nakukumbusha kama ulifundwa najua unakumbuka alichokuambia somo yako: “Kamnyenyekee mumeo, kampende, kamtunze, kamheshimu kwa sababu ndiye kichwa cha familia, baba wa wanao na mkwe wa wazazi wako”. Ukimheshimu, ukampenda na kumthamini naye atajifunza kutoka kwako na mtaishi kwa amani.

Usimtie aibu somo yako kwa kwenda kuusokotola unyago...!